Kutoka 16

Kutoka 16

Mana na kware

1Jumuiya yote ya Waisraeli wakaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri.

2Huko jangwani, jumuiya yote wakawanungʼunikia Musa na Haruni.

3Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungekufa kwa mkono wa Bwana huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”

4Kisha Bwana akamwambia Musa, “Tazama! Nitawanyeshea mikate kutoka mbinguni. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu.

5Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”

6Kwa hiyo Musa na Haruni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kuwa Bwana ndiye aliwatoa Misri,

7kisha asubuhi mtauona utukufu wa Bwana , kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?”

8Kisha Musa akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Bwana wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya Bwana .”

9Kisha Musa akamwambia Haruni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Bwana , kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ”

10Haruni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Bwana ukitokeza katika wingu.

11Bwana akamwambia Musa,

12“Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

13Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na utando wa umande kuzunguka kambi.

14Umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya mchanga wa jangwa.

15Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani.

Musa akawaambia, “Huu ndio mkate ambao Bwana amewapa mle.

16Hivi ndivyo Bwana ameamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi moja kwa kila mtu mliye naye katika hema lenu.’ ”[#16:16 yaani omeri moja, sawa na kilo mbili]

17Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa; baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu.

18Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.

19Kisha Musa akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote hadi asubuhi.”

20Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Musa, wakahifadhi kiasi fulani hadi asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Musa akawakasirikia.

21Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka.

22Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Musa.

23Musa akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana : ‘Kesho itakuwa Sabato ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Bwana . Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke hadi asubuhi.’ ”

24Kwa hiyo wakavihifadhi hadi asubuhi, kama Musa alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu.

25Musa akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Bwana . Hamtapata chochote juu ya nchi leo.

26Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwa chochote.”

27Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote.

28Ndipo Bwana akamwambia Musa, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu hadi lini?

29Fahamuni kuwa Bwana amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.”

30Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.

31Waisraeli wakaita ile mikate mana. Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama, na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali.[#16:31 maana yake mkate kutoka mbinguni]

32Musa akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana : ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”

33Kwa hiyo Musa akamwambia Haruni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Bwana ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

34Kama Bwana alivyomwagiza Musa, hatimaye Haruni aliiweka ile mana ndani ya Sanduku la Ushuhuda ili aweze kuihifadhi.

35Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.

36(Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.)[#16:36 Efa moja ni sawa na kilo 22.]

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.