The chat will start when you send the first message.
1Jumuiya yote ya Israeli ikaondoka kutoka Jangwa la Sini, ikisafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kama Bwana alivyoagiza. Wakapiga kambi huko Refidimu, lakini hapakuwa na maji ya watu kunywa.
2Kwa hiyo wakagombana na Musa wakisema, “Tupe maji ya kunywa.”
Musa akajibu, “Mbona mnagombana nami? Kwa nini mnamjaribu Bwana ?”
3Lakini watu walikuwa na kiu huko, wakanungʼunika dhidi ya Musa, wakisema, “Kwa nini ulitutoa kule Misri, ukatuleta hapa utuue kwa kiu sisi, watoto wetu na mifugo yetu?”
4Kisha Musa akamlilia Bwana , akasema, “Niwafanyie nini watu hawa? Sasa wanakaribia kunipiga kwa mawe.”
5Bwana akamjibu Musa, “Nenda mbele ya watu. Wachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa Israeli, na uchukue mkononi mwako ile fimbo uliyopiga nayo Mto Naili, nawe uende.
6Huko nitasimama mbele yako karibu na mwamba wa Horebu. Uupige mwamba na maji yatatoka ndani yake kwa ajili ya watu kunywa.” Kwa hiyo Musa akafanya haya mbele ya wazee wa Israeli.
7Naye akapaita mahali pale Masa na Meriba, kwa sababu Waisraeli waligombana na kumjaribu Bwana wakisema, “Je, Bwana yu pamoja nasi au la?”[#17:7 maana yake Kujaribu; #17:7 maana yake Kugombana]
8Waamaleki wakaja na kuwashambulia Waisraeli huko Refidimu.
9Musa akamwambia Yoshua, “Chagua baadhi ya watu wetu na uende kupigana na Waamaleki. Kesho nitasimama juu ya kilima nikiwa na fimbo ya Mungu mkononi mwangu.”
10Kwa hiyo Yoshua akapigana na Waamaleki kama Musa alivyomwagiza, nao Musa, Haruni na Huri wakapanda juu ya kilima.
11Ikawa wakati wote Musa alipokuwa amenyanyua mikono yake, Waisraeli walikuwa wakishinda, lakini kila aliposhusha mikono yake Waamaleki walishinda.
12Mikono ya Musa ilipochoka, wakachukua jiwe na kumpa alikalie. Haruni na Huri wakaishikilia juu mikono ya Musa, mmoja upande huu na mwingine upande huu. Wakaitegemeza mikono yake ikabaki thabiti hadi jua lilipozama.
13Kwa hiyo Yoshua akalishinda jeshi la Waamaleki kwa upanga.
14Kisha Bwana akamwambia Musa, “Andika mambo haya katika kitabu ili yakumbukwe, na uhakikishe kwamba Yoshua amesikia, kwa sababu nitafuta kabisa kumbukumbu la Amaleki chini ya mbingu.”
15Musa akajenga madhabahu na kuiita Yehova Nisi.[#17:15 maana yake ni Bendera yangu]
16Musa akasema, “Kwa maana mikono iliinuliwa dhidi ya kiti cha enzi cha Bwana , sasa Bwana atakuwa na vita dhidi ya Waamaleki kizazi hadi kizazi.”