Hosea 14

Hosea 14

Toba iletayo baraka

1Rudi, ee Israeli, kwa Bwana Mungu wako.

Dhambi zako zimekuwa anguko lako!

2Chukueni maneno pamoja nanyi,

mkamrudie Bwana .

Mwambieni:

“Samehe dhambi zetu zote

na utupokee kwa neema,

ili tuweze kutoa matunda yetu

kama sadaka za mafahali.

3Ashuru hawezi kutuokoa,

hatutapanda farasi wa vita.

Kamwe hatutasema tena ‘miungu yetu’

kwa kile ambacho mikono yetu wenyewe imetengeneza,

kwa kuwa kwako wewe yatima hupata huruma.”

4“Nitaponya ukaidi wao

na kuwapenda kwa hiari yangu,

kwa kuwa hasira yangu imeondoka kwao.

5Nitakuwa kama umande kwa Israeli;

atachanua kama yungiyungi.

Kama mwerezi wa Lebanoni

atashusha mizizi yake chini;

6matawi yake yatatanda.

Fahari yake itakuwa kama mti wa mzeituni,

harufu yake nzuri kama mwerezi wa Lebanoni.

7Watu wataishi tena kwenye kivuli chake.

Atastawi kama nafaka.

Atachanua kama mzabibu,

nao umaarufu wake utakuwa

kama divai inayotoka Lebanoni.

8Ee Efraimu, nina shughuli gani tena na sanamu?

Nitamjibu na kumtunza.

Mimi ni kama msunobari wenye majani mabichi;

kuzaa kwako matunda kunatoka kwangu.”

9Ni nani mwenye hekima? Atayatambua mambo haya.

Ni nani mwenye ufahamu? Huyu atayaelewa.

Njia za Bwana ni adili;

wenye haki huenda katika njia hizo,

lakini waasi watajikwaa ndani yake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.