Isaya 24

Isaya 24

Dunia kuharibiwa

1Tazama, Bwana ataifanya dunia kuwa ukiwa

na kuiharibu,

naye atauharibu uso wake

na kutawanya wanaoishi ndani yake:

2ndivyo itakavyokuwa

kwa makuhani na kwa watu,

kwa bwana na kwa mtumishi,

kwa bibi na kwa mjakazi wake,

kwa muuzaji na kwa mnunuzi,

kwa mkopaji na kwa mkopeshaji,

kwa mdaiwa na kwa mdai.

3Dunia itaharibiwa kabisa

na kutekwa nyara kabisa.

Bwana amesema neno hili.

4Dunia inakauka na kunyauka,

dunia inanyongʼonyea na kunyauka,

waliotukuzwa wa dunia wananyongʼonyea.

5Dunia imetiwa unajisi na watu wake;

wameacha kutii sheria,

wamevunja amri

na kuvunja agano la milele.

6Kwa hiyo laana inaiteketeza dunia,

watu wake lazima waichukue hatia yao.

Kwa hiyo wakazi wa dunia wameteketezwa,

nao waliosalia ni wachache sana.

7Divai mpya inakauka na mzabibu unanyauka,

watu wote wafurahishao wanalia kwa huzuni.

8Furaha ya matoazi imekoma,

kelele za wenye furaha zimekoma,

shangwe za kinubi zimenyamaza.

9Hawanywi tena mvinyo pamoja na wimbo,

kileo ni kichungu kwa wanywaji wake.

10Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa,

mlango wa kila nyumba umefungwa.

11Barabarani wanalilia kupata mvinyo,

furaha yote imegeuka kuwa majonzi,

furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.

12Mji umeachwa katika uharibifu,

lango lake limevunjwa vipande.

13Ndivyo itakavyokuwa duniani

na miongoni mwa mataifa,

kama vile wakati mzeituni upigwavyo,

au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.

14Wanapaza sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha,

kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana .

15Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu,

liadhimisheni jina la Bwana , Mungu wa Israeli,

katika visiwa vya bahari.

16Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji:

“Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.”

Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika!

Ole wangu!

Watenda hila wanasaliti!

Kwa hila watenda hila wanasaliti!”

17Hofu, shimo na mtego vinakungojea,

ewe mtu ukaaye duniani.

18Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu

atatumbukia shimoni,

naye yeyote apandaye kutoka shimoni,

atanaswa kwenye mtego.

Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa,

misingi ya dunia inatikisika.

19Dunia imepasuka,

dunia imechanika,

dunia imetikiswa kabisa.

20Dunia inapepesuka kama mlevi,

inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo;

imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake

na ikianguka kamwe haitainuka tena.

21Katika siku ile Bwana ataadhibu

mamlaka zilizo juu mbinguni,

na wafalme walio chini duniani.

22Watakusanywa pamoja

kama wafungwa waliofungwa gerezani;

watafungiwa gerezani

na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.

23Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa;

kwa maana Bwana wa majeshi atatawala

juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu,

tena mbele ya wazee wake, kwa utukufu.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.