The chat will start when you send the first message.
1Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramu, na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.[#7:1 yaani Shamu]
2Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo mioyo ya Ahazi na watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.
3Ndipo Bwana akamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi.[#7:3 maana yake Mabaki Watarudi]
4Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia.
5Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga njama ili wakuangamize, wakisema,
6“Tuishambulie Yuda, naam, tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu, na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.”
7Lakini Bwana Mwenyezi asema hivi:
“ ‘Jambo hili halitatendeka,
halitatukia,
8kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski,
na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake.
Katika muda wa miaka sitini na tano,
Efraimu atakuwa ameharibiwa
kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.
9Kichwa cha Efraimu ni Samaria,
na kichwa cha Samaria
ni mwana wa Remalia peke yake.
Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu,
hamtaimarika kamwe.’ ”
10Bwana akasema na Ahazi tena,
11“Mwombe Bwana Mungu wako ishara, iwe kwenye vina virefu sana, au kwenye vimo virefu sana.”
12Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribu Bwana .”
13Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia?
14Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.[#7:14 maana yake Mungu yu pamoja nasi]
15Atakula jibini na asali atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua mema.
16Lakini kabla mtoto hajajua kukataa mabaya na kuchagua mema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa.
17Bwana ataleta juu yako pamoja na watu wako na juu ya nyumba ya baba yako, nyakati ambazo hazijawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda: naye Bwana atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”
18Katika siku ile Bwana atawapigia filimbi inzi kutoka vijito vya mbali vya Misri, na nyuki kutoka nchi ya Ashuru.
19Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye miteremko, na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba, na kwenye mashimo yote ya maji.
20Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ngʼambo ya Mto, yaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako na malaika ya miguu yako, na kuziondoa ndevu zako pia.[#7:20 yaani Mto Frati]
21Katika siku ile, mtu atahifadhi hai mtamba mmoja na kondoo wawili.
22Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali.
23Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli elfu moja za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu.[#7:23 Shekeli 1,000 ni kama kilo 11.5.]
24Watu wataenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba.
25Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtaenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba. Patakuwa mahali ngʼombe wataachiwa huru, na kondoo kukimbia kimbia.