Isaya 8

Isaya 8

Isaya na wanawe kama ishara

1Bwana akaniambia, “Chukua kitabu kikubwa, uandike kwa kalamu ya kawaida jina: Maher-Shalal-Hash-Bazi.[#8:1 maana yake Haraka kuteka nyara, upesi kwenye hizo nyara]

2Nami nitawaita kuhani Uria, na Zekaria mwana wa Yeberekia kama mashahidi wangu waaminifu.”

3Kisha nikaenda kwa nabii mke, naye akapata mimba, akazaa mwana. Kisha Bwana akaniambia, “Mwite huyo mtoto Maher-Shalal-Hash-Bazi.

4Kabla mtoto hajaweza kusema ‘Baba yangu’ au ‘Mama yangu,’ utajiri wa Dameski na nyara za Samaria zitachukuliwa na mfalme wa Ashuru.”

5Bwana akasema nami tena:

6“Kwa sababu watu hawa wamekataa maji ya Shilo yanayotiririka taratibu

wakamfurahia Resini na mwana wa Remalia;

7kwa hiyo Bwana yu karibu kuleta dhidi yao

mafuriko makubwa ya Mto:

yaani mfalme wa Ashuru na fahari yake yote.

Yatafurika juu ya mifereji yake yote,

yatamwagikia juu ya kingo zake zote,

8na kufika hadi Yuda, yakizunguka kwa kasi juu yake,

yakipita katikati na yakifika hadi shingoni.

Mabawa yake yaliyokunjuliwa

yatafunika upana wa nchi yako,

Ee Imanueli!”

9Inueni ukelele wa vita, enyi mataifa,

na mkavunjwevunjwe!

Sikilizeni, enyi nyote nchi za mbali.

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

Jiandaeni kwa vita, nanyi mkavunjwevunjwe!

10Wekeni mikakati yenu, lakini itashindwa;

fanyeni mipango yenu, lakini haitafanikiwa,

kwa maana Mungu yu pamoja nasi.

11Bwana alisema nami mkono wake wenye nguvu ukiwa juu yangu, akinionya nisifuate njia za taifa hili. Akasema:

12“Usiite fitina kila kitu ambacho watu hawa hukiita fitina,

usiogope kile wanachokiogopa,

wala usikihofu.

13Bwana wa majeshi ndiye peke yake

ikupasaye kumheshimu kuwa mtakatifu,

ndiye peke yake utakayemwogopa,

ndiye peke yake utakayemhofu,

14naye atakuwa mahali patakatifu;

lakini kwa nyumba zote mbili za Israeli atakuwa

jiwe lile linalosababisha watu kujikwaa

na mwamba wa kuwaangusha.

Kwa watu wa Yerusalemu,

atakuwa mtego na tanzi.

15Wengi wao watajikwaa;

wataanguka na kuvunjika,

watategwa na kunaswa.”

16Funga ushuhuda na kutia muhuri sheria

miongoni mwa wanafunzi wangu.

17Nitamngojea Bwana ,

ambaye ameificha nyumba ya Yakobo uso wake.

Nitaliweka tumaini langu kwake.

18Niko hapa, pamoja na watoto ambao Bwana amenipa. Sisi ni ishara na mfano wake katika Israeli, kutoka kwa Bwana wa majeshi, anayeishi juu ya Mlima Sayuni.

19Watu wanapowaambia ninyi kutafuta ushauri kwa waaguzi na wenye kuongea na mizimu, ambao hunongʼona na kunungʼunika, je, watu wasingeuliza kwa Mungu wao? Kwa nini watake shauri kwa wafu kwa ajili ya walio hai?

20Kwa sheria na kwa ushuhuda! Kama hawatasema sawasawa na neno hili, hawana mwanga wa mapambazuko.

21Watazunguka katika nchi yote, wakiwa na dhiki na njaa. Watakapotaabika kwa njaa, watapatwa na hasira kali, nao, wakiwa wanatazama juu, watamlaani mfalme wao na Mungu wao.

22Kisha wataangalia duniani na kuona tu dhiki na giza, hofu na huzuni tupu, nao watasukumiwa kwenye giza nene kabisa.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.