The chat will start when you send the first message.
1Kisha neno la Bwana likanijia:
2“Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.”
3Kwa maana hili ndilo asemalo Bwana kuhusu wana wa kiume na wa kike wanaozaliwa katika nchi hii, na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao, na wale wanaume ambao ni baba zao:
4“Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa, lakini watakuwa kama kinyesi juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa. Mizoga yao itakuwa chakula cha ndege na wanyama wa porini.”
5Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana : “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga; usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeondoa amani yangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asema Bwana .
6“Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, na hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao.
7Hakuna yeyote atakayewapa chakula ili kuwafariji wanaoomboleza kwa ajili ya waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, wala hakuna yeyote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.
8“Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu, na kuketi humo ili kula na kunywa.
9Kwa kuwa hili ndilo asemalo Bwana wa majeshi, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako, nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, na pia sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’
10“Utakapowaambia watu hawa mambo haya yote na wakakuuliza, ‘Kwa nini Bwana ameamuru maafa makubwa kama haya dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi ya Bwana , Mungu wetu?’
11Basi waambie, ‘Ni kwa sababu baba zenu waliniacha mimi, wakafuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu. Waliniacha mimi na hawakuishika sheria yangu,’ asema Bwana .
12‘Lakini ninyi mmetenda uovu kupita baba zenu. Tazama jinsi kila mmoja wenu anafuata ukaidi wa moyo wake mbaya, badala ya kunitii mimi.
13Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwatupa katika nchi ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua, na huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, kwa maana sitawapa fadhili zangu.’
14“Hata hivyo, siku zinakuja,” asema Bwana , “wakati watu hawatasema tena, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’
15bali watasema, ‘Hakika kama Bwana aishivyo, aliyewatoa Waisraeli kutoka nchi ya kaskazini na nchi zote alizokuwa amewafukuzia.’ Maana nitawarudisha katika nchi niliyowapa baba zao.
16“Lakini sasa nitawaagiza wavuvi wengi,” asema Bwana , “nao watawavua. Baada ya hilo, nitawaagizia wawindaji wengi, nao watawawinda kwenye kila mlima na kilima, na katika nyufa za miamba.
17Macho yangu yanaziona njia zao zote, hazikufichika kwangu, wala dhambi yao haikusitirika.
18Nitawalipiza maradufu kwa ajili ya uovu wao na dhambi yao, kwa sababu wameinajisi nchi yangu kwa maumbo yasiyo na uhai ya vinyago vyao vibaya, na kuujaza urithi wangu na sanamu za kuchukiza.”
19Ee Bwana , nguvu zangu na ngome yangu,
kimbilio langu wakati wa taabu,
kwako mataifa watakujia
kutoka miisho ya dunia na kusema,
“Baba zetu hawakuwa na chochote isipokuwa miungu ya uongo,
sanamu batili
ambazo hazikuwafaidi kitu.
20Je, watu hujitengenezea miungu yao wenyewe?
Lakini hiyo si Mungu!”
21“Kwa hiyo nitawafundisha:
wakati huu nitawafundisha
nguvu zangu na uwezo wangu.
Ndipo watajua
kuwa Jina langu ndimi Bwana .