Yeremia 42

Yeremia 42

Yeremia ashauri walionusurika wasihame Yuda

1Ndipo maafisa wote wa jeshi, pamoja na Yohanani mwana wa Karea, na Yezania mwana wa Hoshaya, na watu wote kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana wakamjia

2Yeremia nabii na kumwambia, “Tafadhali sikia maombi yetu na umwombe Bwana Mungu wako kwa ajili ya watu hawa wote waliosalia. Kwa kuwa kama unavyoona sasa, ingawa wakati fulani tulikuwa wengi, sasa tumesalia wachache tu.

3Omba ili Bwana Mungu wako atuambie twende wapi na tufanye nini.”

4Nabii Yeremia akajibu, “Nimewasikia. Kwa hakika nitamwomba Bwana Mungu wenu kama mlivyoomba. Nitawaambia kila kitu asemacho Bwana , wala sitawaficha chochote.”

5Kisha wakamwambia Yeremia, “Bwana na awe shahidi mwaminifu na wa kweli dhidi yetu, ikiwa hatutafanya kila kitu jinsi Bwana Mungu wako atakachokutuma utuambie.

6Likiwa jema au likiwa baya, tutamtii Bwana Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake, ili mambo yote yawe mema kwetu, kwa maana tutamtii Bwana Mungu wetu.”

7Baada ya siku kumi, neno la Bwana likamjia Yeremia.

8Kwa hiyo akawaita Yohanani mwana wa Karea, maafisa wote wa jeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote kuanzia mdogo kabisa hadi aliye mkuu sana.

9Akawaambia, “Hili ndilo asemalo Bwana , Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kuwasilisha maombi yenu:

10‘Mkikaa katika nchi hii, nitawajenga wala sitawabomoa, nitawapanda wala sitawangʼoa, kwani ninahuzunishwa na maafa niliyowapiga nayo.

11Msimwogope mfalme wa Babeli, ambaye sasa mnamwogopa. Msimwogope, asema Bwana , kwa kuwa niko pamoja nanyi, nami nitawaokoa na kuwaponya kutoka mkononi mwake.

12Nitawaonea huruma ili naye awe na huruma kwenu na kuwarudisha katika nchi yenu.’

13“Lakini mkisema, ‘Hatutakaa katika nchi hii,’ hivyo mkaacha kumtii Bwana Mungu wenu,

14na kama mkisema, ‘Hapana, tutaenda kuishi Misri, mahali ambapo hatutaona vita au kusikia sauti ya tarumbeta, au kuwa na njaa ya chakula,’

15basi sikieni neno la Bwana , enyi mabaki ya Yuda. Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Ikiwa mmekusudia kwenda Misri na kufanya makazi huko,

16basi ule upanga mnaouogopa utawapata huko, na njaa mnayoihofia itawafuata huko Misri, nanyi mtafia huko.

17Naam, wote waliokusudia kwenda kuishi Misri watakufa kwa upanga, njaa na tauni; hakuna hata mmoja wao atakayenusurika au kuokoka maafa nitakayoyaleta juu yao.’

18Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo: ‘Kama vile hasira yangu na ghadhabu yangu ilivyomwagwa juu ya wale walioishi Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu mtakapoenda Misri. Mtakuwa kitu cha kulaaniwa na kutishiwa, cha kuhukumiwa, na cha kuaibisha; nanyi hamtapaona mahali hapa tena.’

19“Enyi mabaki ya Yuda, Bwana amewaambia, ‘Msiende Misri.’ Hakikisheni jambo hili: Ninawaonya leo

20kwamba mmefanya kosa kubwa mioyoni mwenu mliponituma kwa Bwana Mungu wenu na kusema, ‘Mwombe Bwana Mungu wetu kwa ajili yetu, nawe utuambie kila kitu atakachosema, nasi tutafanya.’

21Nimewaambieni leo, lakini bado ninyi hamtaki kumtii Bwana Mungu wenu katika yote aliyonituma niwaambie.

22Basi sasa, hakikisheni jambo hili: Mtakufa kwa upanga, njaa na tauni mahali pale mnataka kwenda kuishi.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.