Yeremia 43

Yeremia 43

Yeremia apelekwa Misri

1Yeremia alipomaliza kuwaambia watu maneno yote ya Bwana Mungu wao, yaani kila kitu Bwana alichokuwa amemtuma kuwaambia,

2Azaria mwana wa Hoshaya, na Yohanani mwana wa Karea, na watu wote wenye kiburi wakamwambia Yeremia, “Wewe unasema uongo! Bwana Mungu wetu hajakutuma kusema, ‘Kamwe msiende Misri kukaa huko.’

3Lakini Baruku mwana wa Neria anakuchochea dhidi yetu ili ututie mikononi mwa Wakaldayo, ili watuue au watuchukue uhamishoni Babeli.”

4Basi Yohanani mwana wa Karea, na maafisa wote wa jeshi, na watu wote wakakataa kutii amri ya Bwana ya kukaa katika nchi ya Yuda.

5Badala yake, Yohanani mwana wa Karea na maafisa wote wa jeshi wakawaongoza mabaki yote ya Yuda waliokuwa wamerudi kuishi katika nchi ya Yuda kutoka mataifa yote ambayo walikuwa wametawanywa.

6Pia wakawaongoza wanaume wote, wanawake na watoto, na binti za mfalme ambao Nebuzaradani mkuu wa askari walinzi wa mfalme alikuwa amewaacha na Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani, na nabii Yeremia, na Baruku mwana wa Neria.

7Kwa hiyo wakaingia Misri kwa kutokumtii Bwana , wakaenda hadi Tapanesi.

8Huko Tapanesi neno la Bwana likamjia Yeremia kusema:

9“Wayahudi wakiwa wanaona, chukua baadhi ya mawe makubwa na kuyazika katika udongo wa mfinyanzi katika njia iliyojengwa kwa matofali katika lango la jumba la kifalme la Farao huko Tapanesi.

10Kisha uwaambie, ‘Hili ndilo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asemalo: Nitamtumania mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli, nami nitakiweka kiti chake cha utawala juu ya haya mawe niliyoyazika hapa, naye atatandaza hema lake la ufalme juu yake.

11Atakuja na kuishambulia Misri; atawaua waliokusudiwa kuuawa, atawateka waliokusudiwa kutekwa, na atawaua kwa upanga waliokusudiwa kuuawa kwa upanga.

12Atachoma moto mahekalu ya miungu ya Misri, atachoma mahekalu yao na kuteka miungu yao. Kama mchungaji ajizungushiavyo vazi lake, ndivyo atakavyojizungushia Misri na kuondoka mahali hapo kwa amani.

13Huko, ndani ya hekalu la jua nchini Misri, atabomoa nguzo za ibada, na kuteketeza kwa moto mahekalu ya miungu ya Misri.’ ”[#43:13 yaani Heliopoli ( Mji wa Jua )]

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.