The chat will start when you send the first message.
1Siku sita kabla ya Pasaka, Yesu alienda Bethania, makao ya Lazaro, aliyekuwa amemfufua kutoka kwa wafu.
2Wakaandaa karamu kwa heshima ya Yesu. Martha akawahudumia, wakati Lazaro alikuwa miongoni mwa waliokaa mezani pamoja na Yesu.
3Kisha Mariamu akachukua chupa ya painti moja yenye manukato ya nardo safi ya thamani kubwa, akayamimina miguuni mwa Yesu na kuifuta kwa nywele zake. Nyumba nzima ikajaa harufu nzuri ya manukato.[#12:3 painti moja ni kama nusu lita; #12:3 aina ya mafuta yaliyokuwa yanatengenezwa kutokana na mimea yenye mizizi inayotoa harufu nzuri]
4Ndipo Yuda Iskariote mwana wa Simoni, mmoja wa wanafunzi wa Yesu, ambaye baadaye angemsaliti Yesu, akasema,
5“Kwa nini manukato haya hayakuuzwa kwa dinari mia tatu, na fedha hizo wakapewa maskini?”[#12:5 Dinari 300 ni sawa na mshahara wa kibarua wa siku 300.]
6Yuda hakusema hivi kwa kuwa aliwajali maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwizi; ndiye alikuwa akitunza mfuko wa fedha, na akawa akiiba zile fedha.
7Yesu akasema, “Mwacheni. Aliyanunua manukato hayo ili ayaweke kwa ajili ya siku ya maziko yangu.
8Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini mimi hamtakuwa nami siku zote.”
9Umati mkubwa wa Wayahudi walipojua kwamba Yesu alikuwa huko Bethania, walikuja si tu kwa ajili ya Yesu, lakini pia kumwona Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua.
10Kwa hiyo viongozi wa makuhani wakapanga njama ya kumuua Lazaro pia,
11kwa kuwa kutokana na habari za kufufuliwa kwake, Wayahudi wengi walikuwa wanamfuata Yesu na kumwamini.
12Siku iliyofuata umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekuja kwenye Sikukuu walisikia kwamba Yesu angekuja Yerusalemu.
13Basi wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki, huku wakipaza sauti wakisema,
“Hosana!”
“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”
“Amebarikiwa mfalme wa Israeli!”
14Yesu akamkuta mwana-punda, akampanda, kama ilivyoandikwa,
15“Usiogope, ewe Binti Sayuni;
tazama, mfalme wako anakuja,
amepanda mwana-punda!”
16Wanafunzi wake Yesu mwanzoni hawakuelewa mambo haya. Lakini Yesu alipotukuzwa, ndipo walipokumbuka kuwa mambo haya yalikuwa yameandikwa kwa ajili yake na alitendewa yeye.
17Wale waliokuwepo Yesu alipomwita Lazaro kutoka kaburini na kumfufua kutoka kwa wafu waliendelea kushuhudia.
18Na kwa sababu walikuwa wamesikia kwamba alikuwa ametenda muujiza huu, umati wa watu wakaenda kumlaki.
19Hivyo Mafarisayo walipoona hayo, wakaambiana, “Mnaona, hamwezi kufanya lolote. Angalieni, ulimwengu wote unamfuata yeye!”
20Basi palikuwa Wayunani fulani miongoni mwa wale waliokuwa wameenda kuabudu wakati wa Sikukuu.
21Hawa wakaenda kwa Filipo, aliyekuwa raia wa Bethsaida huko Galilaya, wakiwa na ombi. Wakamwambia, “Tungependa kumwona Yesu.”
22Filipo akaenda akamweleza Andrea, nao wote wawili wakamwambia Yesu.
23Yesu akawajibu, “Saa imewadia ya Mwana wa Adamu kutukuzwa.
24Amin, amin nawaambia, mbegu ya ngano isipoanguka ardhini na kufa, hubakia kama mbegu peke yake. Lakini ikifa, huzaa mbegu nyingi.
25Mtu yeyote anayependa maisha yake atayapoteza, naye ayachukiaye maisha yake katika ulimwengu huu atayaokoa hata kwa uzima wa milele.
26Mtu yeyote akinitumikia lazima anifuate, nami mahali nilipo ndipo mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu akinitumikia, Baba yangu atamheshimu.
27“Sasa roho yangu imefadhaika sana. Niseme nini? ‘Baba, niokoe katika saa hii’? Lakini ni kwa kusudi hili nimeufikia wakati huu.
28Baba, litukuze jina lako.”
Ndipo ikaja sauti kutoka mbinguni, ikasema, “Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.”
29Umati ule wa watu waliokuwa mahali pale waliisikia ile sauti, nao wakasema hiyo ilikuwa sauti ya radi; wengine wakasema malaika ameongea naye.
30Yesu akawaambia, “Sauti hii imesikika kwa faida yenu, wala si kwa faida yangu.
31Sasa ni saa ya hukumu kwa ajili ya ulimwengu huu, sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32Lakini mimi, nikiinuliwa kutoka nchi, nitawavuta watu wote waje kwangu.”
33Yesu aliyasema haya akionesha ni kifo gani atakachokufa.
34Umati ule wa watu wakapaza sauti, wakasema, “Tumesikia kutoka Sheria kwamba Kristo adumu milele; hivyo wewe wawezaje kusema, ‘Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa juu’? Huyu ‘Mwana wa Adamu’ ni nani?”[#12:34 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]
35Ndipo Yesu akawaambia, “Bado kitambo kidogo nuru ingali pamoja nanyi. Nendeni maadamu mna nuru, msije mkakumbwa na giza. Mtu anayetembea gizani hajui anakoenda.
36Wekeni tumaini lenu katika nuru hiyo ili mpate kuwa wana wa nuru.” Baada ya kusema haya, Yesu aliondoka, akajificha wasimwone.
37Hata baada ya Yesu kufanya miujiza hii yote mbele yao, bado hawakumwamini.
38Hili lilikuwa ili kutimiza lile neno la nabii Isaya lililosema:
“Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu,
na mkono wa Bwana umefunuliwa kwa nani?”
39Kwa hivyo hawakuamini, kwa sababu Isaya anasema mahali pengine:
40“Amewafanya vipofu,
na kuifanya mioyo yao kuwa migumu,
ili wasiweze kuona kwa macho yao,
wala kuelewa kwa mioyo yao,
wasije wakageuka nami nikawaponya.”
41Isaya alisema haya alipoona utukufu wa Yesu na kunena habari zake.
42Lakini wengi miongoni mwa viongozi wa Wayahudi walimwamini, lakini kwa sababu ya Mafarisayo hawakukiri waziwazi kwa maana waliogopa kufukuzwa katika masinagogi.
43Wao walipenda sifa za wanadamu kuliko sifa zinazotoka kwa Mungu.
44Yesu akapaza sauti akasema, “Yeyote aniaminiye, haniamini mimi peke yangu, bali pia yeye aliyenituma.
45Yeyote anionaye mimi amemwona yeye aliyenituma.
46Mimi nimekuja kama nuru ulimwenguni, ili kila mtu aniaminiye asibaki gizani.
47“Mimi simhukumu mtu yeyote anayesikia maneno yangu na asiyatii, kwa maana sikuja kuuhukumu ulimwengu, bali kuuokoa.
48Yuko anayehukumu yule anayenikataa mimi na kuyakataa maneno yangu; yale maneno niliyoyasema yenyewe yatamhukumu siku ya mwisho.
49Kwa maana sisemi kwa ajili yangu mwenyewe, bali Baba aliyenituma aliniamuru ni nini cha kusema na jinsi ya kukisema.
50Nami ninajua amri zake huongoza hadi kwenye uzima wa milele. Hivyo lolote nisemalo, ndilo lile Baba aliloniambia niseme.”