Yohana 19

Yohana 19

Yesu ahukumiwa kusulubiwa

(Mt 27:15‑31; Mk 15:6‑20; Lk 23:13‑25)

1Ndipo Pilato akamtoa Yesu akaamuru apigwe mijeledi.

2Askari wakasokota taji la miiba, wakamvika Yesu kichwani. Wakamvalisha joho la zambarau.

3Wakawa wanapanda pale alipo tena na tena, wakisema, “Salamu, mfalme wa Wayahudi!” Huku wakimpiga makofi usoni.

4Pilato akatoka tena nje, akawaambia wale waliokusanyika, “Tazameni, namkabidhi Yesu kwenu kuwajulisha kwamba mimi sioni msingi wowote wa kumshtaki.”

5Kwa hiyo Yesu akatoka nje akiwa amevaa lile taji la miiba na lile vazi la zambarau. Pilato akawaambia, “Tazameni, mtu ndiye huyu!”

6Wale viongozi wa makuhani na maafisa walipomwona, wakapiga kelele wakisema, “Msulubishe! Msulubishe!”

Pilato akawaambia, “Mchukueni ninyi mkamsulubishe. Lakini mimi sioni msingi wowote wa kumshtaki.”

7Viongozi wa Wayahudi wakamjibu, “Sisi tunayo sheria, na kutokana na sheria hiyo, hana budi kufa kwa sababu yeye alijiita Mwana wa Mungu.”

8Pilato aliposikia haya, akaogopa zaidi.

9Akaingia tena ndani ya jumba la kifalme, akamuuliza Yesu, “Wewe umetoka wapi?” Lakini Yesu hakumjibu.

10Pilato akamwambia, “Wewe unakataa kuongea na mimi? Hujui ya kuwa nina mamlaka ya kukuachia huru au kukusulubisha?”

11Ndipo Yesu akamwambia, “Wewe hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa kutoka juu. Kwa hiyo yeye aliyenitia mikononi mwako ana hatia ya dhambi iliyo kubwa zaidi.”

12Tangu wakati huo, Pilato akajitahidi kutafuta njia ya kumfungua Yesu, lakini viongozi wa Wayahudi wakazidi kupiga kelele wakisema, “Ukimwachia huyu mtu, wewe si rafiki wa Kaisari. Mtu yeyote anayedai kuwa mfalme anampinga Kaisari.”

13Pilato aliposikia maneno haya, akamtoa Yesu nje tena. Akaketi kwenye kiti chake cha hukumu, mahali palipoitwa Sakafu ya Jiwe (kwa Kiebrania ni Gabatha).

14Basi ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, yapata kama saa sita hivi.

Pilato akawaambia Wayahudi, “Huyu hapa mfalme wenu!”

15Wao wakapiga kelele, “Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!”

Pilato akawauliza, “Je, nimsulubishe mfalme wenu?”

Wale viongozi wa makuhani wakamjibu, “Sisi hatuna mfalme mwingine ila Kaisari.”

16Ndipo Pilato akamkabidhi Yesu kwao ili wamsulubishe.

Yesu asulubishwa

(Mt 27:32‑44; Mk 15:21‑32; Lk 23:26‑43)

Kwa hiyo askari wakamchukua Yesu.

17Yesu, akiwa ameubeba msalaba wake, akatoka kuelekea mahali palipoitwa Fuvu la Kichwa (kwa Kiebrania ni Golgotha).

18Hapo ndipo walipomsulubisha. Pamoja naye walisulubisha watu wawili, mmoja kila upande wake, naye Yesu katikati.

19Pilato akaamuru tangazo liandikwe na liwekwe juu kwenye msalaba wa Yesu; likasema:

20Kwa kuwa mahali hapo Yesu aliposulubiwa palikuwa karibu na mjini, Wayahudi wengi walisoma maandishi haya yaliyokuwa yameandikwa kwa lugha za Kiebrania, Kiyunani na Kilatini.

21Viongozi wa makuhani wa Wayahudi wakapinga, wakamwambia Pilato, “Usiandike ‘Mfalme wa Wayahudi,’ bali andika kwamba mtu huyu alisema yeye ni mfalme wa Wayahudi.”

22Pilato akawajibu, “Nilichokwisha kuandika, nimeandika!”

Mavazi ya Yesu yagawanywa

23Askari walipokwisha kumsulubisha Yesu, walichukua nguo zake wakazigawa mafungu manne, kila askari fungu lake. Ila walikubaliana wasilichane lile vazi lake kwa maana lilikuwa halina mshono, bali limefumwa tangu juu hadi chini.

24Wakaambiana, “Tusilichane ila tulipigie kura ili kuamua ni nani atalichukua.”[#19:24 Za 22:18]

Hili lilitukia ili Maandiko yapate kutimizwa yale yaliyosema,

“Wanagawana nguo zangu,

na vazi langu wanalipigia kura.”

Hayo ndiyo waliyoyafanya wale askari.

25Karibu na msalaba wa Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada wa mamaye, na Mariamu mke wa Klopa, na Mariamu Magdalene.

26Yesu alipomwona mama yake mahali pale, na yule mwanafunzi aliyempenda akiwa amesimama karibu, Yesu akamwambia mama yake, “Mama, huyu hapa ndiye mwanao.”

27Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Nawe huyu hapa ndiye mama yako.” Tangu wakati huo yule mwanafunzi akamchukua mama yake Yesu nyumbani mwake.

Kifo cha Yesu

(Mt 27:45‑56; Mk 15:33‑41; Lk 23:44‑49)

28Baada ya haya, akijua kuwa mambo yote yamemalizika, na ili kutimiza Maandiko, Yesu akasema, “Naona kiu.”

29Hapo palikuwa na bakuli lililojaa siki. Kwa hiyo wakachovya sifongo kwenye hiyo siki, wakaiweka kwenye ufito wa mti wa hisopo, wakampelekea mdomoni.

30Baada ya kuionja hiyo siki, Yesu akasema, “Imekwisha.” Akainamisha kichwa chake, akaitoa roho yake.

Yesu achomwa mkuki ubavuni

31Ilikuwa siku ya Maandalio ya Pasaka, na siku iliyofuata ingekuwa Sabato maalum. Kwa kuwa viongozi wa Wayahudi hawakutaka miili ibaki msalabani siku ya Sabato, wakamwomba Pilato aamuru miguu ya wale waliosulubiwa ivunjwe, na miili iondolewe kwenye misalaba.

32Kwa hiyo askari wakaenda wakavunja miguu ya mtu wa kwanza aliyesulubiwa pamoja na Yesu, na ya yule mwingine pia.

33Lakini walipomkaribia Yesu, wakaona ya kuwa amekwisha kufa, hivyo hawakuvunja miguu yake.

34Badala yake mmoja wa wale askari akamchoma mkuki ubavuni, na mara pakatoka damu na maji.

35Mtu aliyeona mambo hayo ndiye alitoa ushuhuda, nao ushuhuda wake ni kweli. Anajua kuwa anasema kweli, naye anashuhudia ili pia nanyi mpate kuamini.

36Kwa maana mambo haya yalitukia ili andiko litimie, lisemalo, “Hakuna hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa.”[#19:36 Kut 12:46; Hes 9:12; Za 34:20]

37Tena andiko lingine lasema, “Watamtazama yeye waliyemchoma.”[#19:37 Zek 12:10]

Maziko ya Yesu

(Mt 27:57‑61; Mk 15:42‑47; Lk 23:50‑56)

38Baada ya mambo haya, Yusufu wa Arimathaya, aliyekuwa mfuasi wa Yesu, ingawa kwa siri kwa sababu ya kuwaogopa viongozi wa Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili kuuchukua mwili wa Yesu. Pilato alimruhusu, hivyo akaja, akauchukua.

39Naye Nikodemo, yule ambaye kwanza alimwendea Yesu usiku, akaja, akaleta mchanganyiko wa manemane na manukato, yenye uzito wa zaidi ya kilo thelathini.

40Wakauchukua mwili wa Yesu, wakaufunga katika sanda ya kitani safi pamoja na yale manukato, kama ilivyokuwa desturi ya Wayahudi.

41Basi palikuwa na bustani karibu na mahali pale aliposulubiwa, na pale ndani ya ile bustani palikuwa na kaburi jipya, ambalo halikuwa limezikiwa mtu bado.

42Kwa hiyo, kwa kuwa ilikuwa siku ya Wayahudi ya Maandalio, nalo kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamzika Yesu humo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.