Yohana 4

Yohana 4

Yesu azungumza na mwanamke Msamaria

1Yesu alipata habari kuwa Mafarisayo walisikia kwamba yeye alikuwa akipata wanafunzi kuliko Yohana na kuwabatiza,

2ingawa kwa kweli si Yesu mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake.

3Bwana alipojua mambo haya, aliondoka Yudea akarudi tena Galilaya.

4Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria.

5Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu.

6Kisima cha Yakobo kilikuwa huko. Naye Yesu alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.

7Mwanamke mmoja Msamaria alipokuja kuteka maji, Yesu akamwambia, “Naomba maji ninywe.”

8(Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wameenda mjini kununua chakula.)

9Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe maji ya kunywa?” (Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.)

10Yesu akamjibu, “Kama ungeijua karama ya Mungu, na ni nani anakuomba maji ya kunywa, ungemwomba yeye, naye angekupa maji ya uzima.”

11Yule mwanamke akamjibu, “Bwana, wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi?

12Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”

13Yesu akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki ataona kiu tena.

14Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujika uzima wa milele.”

15Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena, wala nisije tena hapa kuteka maji!”

16Yesu akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”

17Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.”

Yesu akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume.

18Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano, na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”

19Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii.

20Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”

21Yesu akamjibu, “Mwanamke, niamini: wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala huko Yerusalemu.

22Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi.

23Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba anawatafuta watu wanaomwabudu kwa namna hii.

24Mungu ni Roho, na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

25Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya” (aitwaye Kristo) “anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”

26Yesu akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”

27Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au, “Kwa nini unazungumza naye?”

28Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini, akawaambia watu,

29“Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Kristo?”[#4:29 maana yake Masiya , yaani Aliyetiwa mafuta.]

30Basi wakamiminika watu kutoka mjini, wakamwendea Yesu.

31Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Rabi, kula.”

32Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”

33Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?”

34Lakini Yesu akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake.

35Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune’? Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa!

36Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja.

37Hivyo ule msemo, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa.

38Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda. Wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”

Wasamaria wengi waamini

39Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Yesu kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.”

40Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili.

41Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.

42Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kwamba huyu ndiye Kristo, Mwokozi wa ulimwengu.”

Yesu amponya mwana wa afisa

43Baada ya zile siku mbili, Yesu aliondoka kwenda Galilaya.

44(Basi Yesu mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.)

45Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.

46Hivyo Yesu akafika tena Kana ya Galilaya, kule alikuwa amebadili maji kuwa divai. Kulikuwa na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu.

47Huyo mtu aliposikia kwamba Yesu alikuwa amewasili Galilaya kutoka Yudea, alimwendea na kumsihi aende akamponye mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.

48Yesu akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”

49Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”

50Yesu akamjibu, “Nenda zako, mwanao yu hai.”

Yule afisa akaamini yale maneno Yesu aliyomwambia, akaenda zake.

51Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake, wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima.

52Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana saa saba, ndipo homa iliisha.”

53Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati Yesu alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Yesu.

54Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Yesu alifanya aliporudi Galilaya kutoka Yudea.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.