Yoshua 8

Yoshua 8

Mji wa Ai waangamizwa

1Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Usiogope, wala usivunjike moyo. Chukua jeshi lote la vita uende pamoja nalo kuishambulia Ai. Kwa kuwa nimeshamweka mikononi mwako mfalme wa Ai, pamoja na watu wake, mji wake na nchi yake.

2Utautendea mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyotendea Yeriko na mfalme wake, isipokuwa mnaweza kunyakua mali zao na mifugo yao kuwa nyara zenu. Weka waviziaji upande wa nyuma ya mji.”

3Basi Yoshua na jeshi lote wakainuka kushambulia Ai. Akachagua mashujaa elfu thelathini walio bora miongoni mwa wapiganaji wake, akawapeleka wakati wa usiku,

4akiwaagiza: “Sikilizeni kwa makini. Mtavizia nyuma ya mji. Msiende mbali sana na mji. Wote kuweni macho.

5Mimi na watu walio pamoja nami tutaukabili mji, kisha itakuwa hapo watu watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo awali, sisi tutawakimbia.

6Watatufuatilia hadi tutakapokuwa tumewavuta mbali na mji kwa kuwa watasema, ‘Wanatukimbia, kama walivyofanya hapo awali.’ Hivyo tutakapowakimbia,

7ninyi mtainuka mtoke mafichoni na kuuteka mji. Bwana Mungu wenu atautia mkononi mwenu.

8Mtakapokuwa mmeuteka mji, uteketezeni kwa moto. Fanyeni kama vile Bwana alivyoamuru. Tazameni, nimewaagiza.”

9Ndipo Yoshua akawatuma watu, nao wakaenda mahali pa kujificha, wakawa wanavizia kati ya Betheli na Ai, kuelekea upande wa magharibi wa Ai, lakini Yoshua akalala miongoni mwa watu usiku huo.

10Asubuhi na mapema siku iliyofuata, Yoshua akakusanya jeshi lake, na yeye na viongozi wa Israeli wakawaongoza kwenda Ai.

11Wanajeshi wote waliokuwa pamoja na Yoshua walipanda, wakakaribia na kufika mbele ya mji. Wakapiga kambi kaskazini mwa Ai, pakiwa na bonde kati yao na huo mji.

12Yoshua alikuwa amewachukua watu wapatao elfu tano, akawaweka mafichoni kusubiri kushambulia, kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa mji.

13Wakawaweka askari katika maeneo yao: wale wote waliokuwa kambini wakawa kaskazini ya mji na wale waliokuwa wakivizia wakawa upande wa magharibi. Usiku huo Yoshua akaenda katika lile bonde.

14Mfalme wa Ai alipoona jambo hili, yeye pamoja na wanaume wote wa mji wakatoka kwa haraka asubuhi na mapema kukutana na Israeli katika vita mahali palipotazamana na Araba. Lakini hakujua kwamba kulikuwa kumewekwa waviziaji dhidi yake nyuma ya mji.

15Yoshua na Waisraeli wote wakaruhusu kurudishwa nyuma mbele yao, na kuelekea jangwani.

16Watu wote wa Ai wakaitwa ili kuwafuatia, nao wakavutwa kumfuatia Yoshua mbali na mji.

17Hakuna hata mwanaume mmoja aliyebakia Ai wala Betheli ambaye hakufuatia Israeli. Wakauacha mji wazi na kuwafuatia Waisraeli.

18Ndipo Bwana akamwambia Yoshua, “Inua huo mkuki ulio mkononi mwako kuuelekeza Ai, kwa kuwa nitautia huo mji mkononi mwako.” Hivyo Yoshua akauelekeza mkuki wake Ai.

19Mara tu alipofanya hivi, wale watu waliokuwa mafichoni wakaondoka upesi kutoka mahali pao na kukimbia mbele. Wakaingia ndani ya mji, wakauteka na kuutia moto kwa haraka.

20Wanaume wa Ai wakaangalia nyuma, wakauona moshi wa huo mji ukielekea angani, lakini hawakuwa na nafasi ya kutoroka kwa upande wowote, kwa kuwa wale Waisraeli waliokuwa wakiwakimbia kuelekea jangwani walikuwa wamegeuka nyuma kuwakabili wakimbizaji wao.

21Basi Yoshua na Waisraeli wote walipoona kwamba waviziaji wameshauteka mji na moshi ulikuwa unapaa juu kwenye mji, wakawageukia wanaume wa Ai na kuwashambulia.

22Wale waviziaji nao pia wakatoka nje ya mji dhidi yao, hivi kwamba wakashikiwa katikati, Waisraeli wakiwa pande zote mbili. Israeli wakawaua, bila kuwaachia yeyote aliyenusurika wala aliyetoroka.

23Lakini wakamchukua mfalme wa Ai akiwa hai na kumleta kwa Yoshua.

24Israeli ilipomaliza kuwaua wanaume wote wa Ai katika mashamba na jangwani walipokuwa wamewafukuzia, na baada ya kila mmoja wao kuuawa kwa upanga, Waisraeli wote wakarudi Ai na kuwaua wale waliokuwa wamebakia mjini.

25Wanaume na wanawake elfu kumi na mbili waliangamia siku ile, yaani watu wote wa Ai.

26Kwa maana Yoshua hakuurudisha ule mkono wake uliokuwa umeuinua mkuki hadi alipomaliza kuwaangamiza wote walioishi Ai.

27Lakini Israeli wakajichukulia mifugo na nyara za mji huu, kama vile Bwana alivyokuwa amemwamuru Yoshua.

28Kwa hiyo Yoshua akauchoma moto mji wa Ai na kuufanya kuwa lundo la magofu la kudumu, mahali pa ukiwa hadi leo.

29Akamwangika mfalme wa Ai kwenye mti na kumwacha hapo hadi jioni. Wakati wa jua kutua, Yoshua akawaamuru wautoe mwili wake kwenye mti na kuutupa kwenye ingilio la lango la mji. Kisha wakalundika mawe mengi makubwa juu yake, ambayo yamesalia hadi leo.

Agano lafanywa upya katika Mlima Ebali

30Kisha Yoshua akajenga madhabahu ya Bwana , Mungu wa Israeli, katika Mlima Ebali,

31kama Musa mtumishi wa Bwana alivyokuwa amewaamuru Waisraeli. Akaijenga sawasawa na ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria ya Musa: madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo juu yake hakuna chombo cha chuma kilichotumika. Hapo juu yake wakamtolea Bwana sadaka za kuteketezwa na kutoa sadaka za amani.[#8:31 yaani sadaka za ushirika]

32Pale mbele ya Waisraeli, Yoshua akanakili juu ya hayo mawe sheria ya Musa, aliyokuwa ameiandika.

33Waisraeli wote, wakiwa na wazee wao, maafisa na waamuzi, walikuwa wamesimama pande zote mbili za Sanduku la Agano la Bwana , wakiwaelekea makuhani Walawi waliokuwa wamelibeba. Wageni walioishi miongoni mwao, pamoja na wazawa, walikuwa hapo. Nusu ya watu walisimama mbele ya Mlima Gerizimu, na nusu nyingine wakasimama mbele ya Mlima Ebali, kama vile Musa mtumishi wa Bwana alivyokuwa ameamuru hapo mwanzo alipotoa maagizo ya kuwabariki watu wa Israeli.

34Hatimaye, Yoshua akasoma maneno yote ya sheria, yaani baraka na laana, kama vile ilivyoandikwa katika Kitabu cha Sheria.

35Hakuna neno lolote katika yale yote ambayo Musa alikuwa ameamuru ambalo Yoshua hakuwasomea kusanyiko lote la Waisraeli, ikiwa ni pamoja na wanawake na watoto, na wageni walioishi miongoni mwao.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.