The chat will start when you send the first message.
1Yesu na wanafunzi wake wakafika upande wa pili wa ziwa, wakaingia katika nchi ya Wagerasi.
2Yesu alipotoka kwenye mashua, mara mtu mmoja mwenye pepo mchafu akatoka makaburini, akakutana naye.
3Mtu huyu aliishi makaburini, wala hakuna aliyeweza kumzuia hata kwa kumfunga minyororo.
4Kwa kuwa mara kwa mara alikuwa amefungwa minyororo mikononi na miguuni, lakini akaikata hiyo minyororo na kuzivunja zile pingu miguuni mwake. Hapakuwa na mtu yeyote aliyekuwa na nguvu za kumzuia.
5Usiku na mchana alikuwa makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikatakata kwa mawe.
6Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akapiga magoti mbele yake.
7Akapaza sauti kwa nguvu akisema, “Una nini nami, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Ninakusihi kwa jina la Mungu, usinitese!”
8Kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, “Mtoke mtu huyu, wewe pepo mchafu!”
9Yesu akamuuliza, “Jina lako ni nani?”
Akamjibu, “Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tuko wengi.”
10Akamsihi Yesu sana asiwapeleke nje ya nchi ile.
11Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe lililokuwa likilisha karibu kando ya kilima.
12Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu wakisema, “Tuamuru twende kwenye wale nguruwe. Turuhusu tuwaingie.”
13Basi Yesu akawaruhusu, nao wale pepo wachafu wakatoka, wakawaingia hao nguruwe. Lile kundi lilikuwa na nguruwe wapatao elfu mbili, nao wote wakateremkia gengeni kwa kasi, nao wakatumbukia ziwani na kuzama.
14Wale watu waliokuwa wakichunga hao nguruwe wakakimbilia mjini na vijijini kueleza yaliyotukia. Watu wakaenda kuona hayo yaliyokuwa yametukia.
15Walipofika kwa Yesu, wakamwona yule mtu aliyekuwa amepagawa na legioni ya pepo wachafu akiwa ameketi hapo, amevaa nguo na mwenye akili timamu. Wakaogopa.
16Wale walioyaona mambo hayo wakawaeleza watu wengine yaliyomtokea yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu, na habari za lile kundi la nguruwe pia.
17Basi watu wakaanza kumwomba Yesu aondoke katika nchi yao.
18Yesu alipokuwa anaingia kwenye mashua, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu akamsihi Yesu waende pamoja.
19Yesu hakumruhusu, bali alimwambia, “Nenda nyumbani kwa jamaa yako ukawaeleze mambo makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokuhurumia.”
20Yule mtu akaenda zake, akaanza kutangaza katika Dekapoli mambo makuu Yesu aliyomtendea. Nao watu wote wakastaajabu.
21Yesu alipokwisha kuvuka tena na kufika ngʼambo, umati mkubwa wa watu wakamzunguka hapo kando ya bahari.
22Kisha mmoja wa viongozi wa sinagogi aliyeitwa Yairo akafika pale. Naye alipomwona Yesu, akapiga magoti miguuni pake,
23akamsihi akisema, “Binti yangu mdogo ni mgonjwa mahututi. Tafadhali nakusihi, njoo uweke mikono yako juu yake ili apate kupona, naye ataishi.”
24Hivyo Yesu akaenda pamoja naye.
Umati mkubwa wa watu wakamfuata, nao watu wakawa wanamsonga.
25Hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na mbili.
26Mwanamke huyu alikuwa ameteseka sana kwa mikono ya matabibu wengi, na kutumia kila kitu alichokuwa nacho. Lakini badala ya kupona, hali yake ilizidi kuwa mbaya.
27Alikuwa amesikia habari za Yesu, naye akaja kwa nyuma yake kwenye umati wa watu, akaligusa vazi lake,
28kwa maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitaponywa.”
29Mara kutoka damu kwake kukakoma, naye akajisikia mwilini mwake amepona kabisa.
30Ghafula Yesu akatambua kuwa nguvu zimemtoka. Akageukia umati wa watu na kuuliza, “Ni nani aliyegusa mavazi yangu?”
31Wanafunzi wake wakamjibu, “Unaona jinsi watu wanavyokusonga. Wawezaje kuuliza, ‘Ni nani aliyenigusa?’ ”
32Lakini Yesu akaangalia pande zote ili aone ni nani aliyemgusa.
33Yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni pake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote.
34Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”
35Alipokuwa bado anaongea, watu wakafika kutoka nyumbani mwa Yairo. Wakamwambia, “Binti yako amekufa. Kwa nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?”
36Aliposikia hayo waliyosema, Yesu akamwambia huyo kiongozi wa sinagogi, “Usiogope. Amini tu.”
37Hakumruhusu mtu yeyote amfuate isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, nduguye Yakobo.
38Walipofika nyumbani mwa yule kiongozi wa sinagogi, Yesu akaona ghasia, watu wakilia na kuomboleza kwa sauti kubwa.
39Alipokwisha kuingia ndani, akawaambia, “Kwa nini mnafanya ghasia na kulia? Mtoto hajafa, bali amelala tu.”
40Wale watu wakamcheka.
Baada ya kuwafukuza wote nje, Yesu akaenda na baba na mama wa yule mtoto, pamoja na wale wanafunzi aliokuwa nao, wakaingia ndani hadi pale alipokuwa mtoto yule.
41Akamshika mtoto mkono, akamwambia, “Talitha koum!” (maana yake, “Msichana, nakuambia: amka!”)
42Mara yule msichana akasimama, akaanza kutembea (alikuwa na umri wa miaka kumi na mbili). Walipoona haya, wakastaajabu sana.
43Yesu akawaagiza kwa ukali wasimweleze mtu yeyote jambo hilo, naye akawaambia wampe yule msichana chakula.