Marko 8

Marko 8

Yesu alisha wanaume 4,000

(Mt 15:32‑39)

1Katika siku hizo, umati mkubwa wa watu walikusanyika tena. Kwa kuwa walikuwa hawana chakula, Yesu akawaita wanafunzi wake akawaambia,

2“Ninahurumia umati huu wa watu, kwa sababu sasa wamekuwa nami kwa muda wa siku tatu na hawana chakula.

3Nikiwaaga waende nyumbani bila kula, watazimia njiani kwa sababu baadhi yao wametoka mbali.”

4Wanafunzi wake wakamjibu, “Lakini hapa nyikani tutapata wapi mikate ya kutosha kuwalisha?”

5Yesu akawauliza, “Mna mikate mingapi?”

Wakajibu, “Tuna mikate saba.”

6Akawaambia watu waketi chini. Akaichukua ile mikate saba na kushukuru, baadaye akaimega na kuwapa wanafunzi wake ili wawagawie watu. Wanafunzi wake wakafanya hivyo.

7Walikuwa pia na visamaki vichache, Yesu akavibariki, akawaamuru wanafunzi wake wawagawie watu.

8Wale watu walikula na kutosheka. Baadaye wanafunzi wakakusanya vipande vilivyosalia, wakajaza vikapu saba.

9Watu waliokula walikuwa wapata elfu nne. Baada ya kuwaaga,

10aliingia kwenye mashua pamoja na wanafunzi wake, akaenda sehemu za Dalmanutha.

Mafarisayo waomba ishara

(Mt 12:38‑42)

11Mafarisayo wakaja, wakaanza kumhoji Yesu. Ili kumtega, wakamwomba awaoneshe ishara kutoka mbinguni.

12Akahuzunika moyoni, akawaambia, “Kwa nini kizazi hiki kinataka ishara? Amin nawaambieni, hakitapewa ishara yoyote.”

13Kisha akawaacha, akarudi kwenye mashua, akavuka hadi ngʼambo.

Chachu ya Mafarisayo na ya Herode

(Mt 16:5‑12)

14Wanafunzi walikuwa wamesahau kuchukua mikate ya kutosha. Walikuwa na mkate mmoja tu kwenye mashua.

15Yesu akawaonya: “Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na ya Herode.”

16Wakajadiliana wao kwa wao, na kusema, “Anasema hivi kwa sababu hatukuleta mikate.”

17Yesu, akifahamu majadiliano yao, akawauliza: “Mbona mnajadiliana kuhusu kutokuwa na mikate? Je, bado hamtambui wala hamwelewi? Je, mbona mioyo yenu ni migumu kiasi hicho?

18Je, mna macho lakini mnashindwa kuona, na mna masikio lakini mnashindwa kusikia? Je, hamkumbuki?

19Nilipoimega ile mikate mitano kwa watu elfu tano, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”

Wakamjibu, “Kumi na viwili.”

20“Je, nilipoimega ile mikate saba kwa watu elfu nne, mlikusanya vikapu vingapi vilivyojaa mabaki?”

Wakamjibu, “Saba.”

21Ndipo akawauliza, “Je, bado hamwelewi?”

Yesu amponya kipofu huko Bethsaida

22Wakafika Bethsaida na baadhi ya watu wakamleta mtu mmoja kipofu wakamsihi Yesu amguse.

23Yesu akamshika mkono huyo kipofu akampeleka nje ya kijiji. Baada ya kuyatemea mate macho ya yule kipofu na kumwekea mikono, Yesu akamuuliza, “Unaona chochote?”

24Yule kipofu akaangalia, akasema, “Ninaona watu, wanaonekana kama miti inayotembea.”

25Yesu akamwekea tena mikono machoni. Kisha macho yake yakafunguka, kuona kwake kukarejea naye akaona kila kitu dhahiri.

26Yesu akamtuma nyumbani mwake, akamwambia, “Hata kijijini usiingie.”

Petro amkiri Yesu kuwa Kristo

(Mt 16:13‑20; Lk 9:18‑21)

27Yesu na wanafunzi wake wakaelekea vijiji vya Kaisaria-Filipi. Walipokuwa njiani, Yesu akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”

28Wakamjibu, “Baadhi husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya, na bado wengine husema wewe ni mmoja wa manabii.”

29Akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo.”

30Yesu akawaonya wasimwambie mtu yeyote habari zake.

Yesu atabiri kifo chake

(Mt 16:21‑28; Lk 9:22‑27)

31Ndipo akaanza kuwafundisha wanafunzi wake kuwa Mwana wa Adamu lazima atapata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani, na walimu wa sheria, na kwamba itampasa auawe lakini baada ya siku tatu afufuliwe.

32Aliyasema haya waziwazi. Ndipo Petro akamchukua kando na akaanza kumkemea.

33Lakini Yesu akageuka na kuwaangalia wanafunzi wake, na akamkemea Petro. Akasema, “Rudi nyuma yangu, Shetani! Moyo wako hauwazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

34Ndipo akawaita umati ule wa watu pamoja na wanafunzi wake, akasema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.

35Kwa maana yeyote anayetaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza, lakini yeyote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili atayaokoa.

36Je, itamfaidi nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?

37Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?

38Mtu yeyote akinionea aibu mimi na maneno yangu katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu naye atamwonea aibu wakati atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.