The chat will start when you send the first message.
1Mfalme wa Aradi, aliyekuwa Mkanaani aliyeishi huko Negebu, aliposikia kwamba Waisraeli walikuwa wanakuja kwa njia ya Atharimu, aliwashambulia Waisraeli na kuwateka baadhi yao.
2Ndipo Israeli akaweka nadhiri hii kwa Bwana : “Ikiwa utawatia watu hawa mikononi mwetu, tutaiangamiza kabisa miji yao.”
3Bwana akasikiliza ombi la Waisraeli, naye akawapa ushindi juu ya Wakanaani. Wakawaangamiza kabisa na miji yao; hivyo mahali pale pakaitwa Horma.[#21:3 maana yake Maangamizi]
4Waisraeli wakasafiri kutoka Mlima Hori kupitia njia inayoelekea Bahari ya Shamu, kuizunguka Edomu. Lakini watu wakakosa uvumilivu njiani,[#21:4 yaani Bahari Nyekundu au Bahari ya Mafunjo]
5wakamnungʼunikia Mungu na Musa, wakisema, “Kwa nini umetupandisha kutoka Misri ili tufe jangwani? Hakuna mkate! Hakuna maji! Nasi tunachukia sana chakula hiki duni!”
6Ndipo Bwana akapeleka nyoka wenye sumu kati yao; wakawauma watu, nao Waisraeli wengi wakafa.
7Watu wakamjia Musa na kusema, “Tumetenda dhambi wakati tuliponena dhidi ya Bwana na dhidi yako. Mwombe Bwana ili atuondolee hawa nyoka.” Hivyo Musa akawaombea hao watu.
8Bwana akamwambia Musa, “Tengeneza nyoka wa shaba na umweke juu ya mti; yeyote aliyeumwa na nyoka anaweza kumtazama na akaishi tena.”
9Kwa hiyo Musa akatengeneza nyoka wa shaba na kumweka juu ya mti. Kisha wakati mtu yeyote aliumwa na nyoka, naye akamtazama yule nyoka wa shaba, aliishi.
10Waisraeli waliendelea na safari yao na wakapiga kambi huko Obothi.
11Kisha wakaondoka Obothi na kupiga kambi huko Iye-Abarimu, katika jangwa linalotazamana na Moabu kuelekea mawio ya jua.
12Kutoka hapo waliendelea mbele wakapiga kambi kwenye Bonde la Zeredi.
13Wakasafiri kutoka hapo na kupiga kambi kando ya Mto Arnoni, ambao uko katika jangwa lililoenea hadi nchi ya Waamori. Mto Arnoni ni mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.
14Ndiyo sababu Kitabu cha Vita vya Bwana kinasema:
“Wahebu nchini Sufa, na mabonde,
Mto Arnoni,
15na miteremko ya mabonde
inayofika hadi makazi ya Ari,
na kuegemea mpakani mwa Moabu.”
16Kutoka hapo waliendelea mbele hadi kisima cha Beeri; kwenye kisima ambacho Bwana alimwambia Musa, “Wakusanye watu pamoja, nami nitawapa maji.”
17Kisha Israeli akaimba wimbo huu:
“Bubujika, ee kisima!
Imba kuhusu maji,
18kuhusu kisima ambacho kilichimbwa na wakuu,
ambacho watu mashuhuri walikifukua,
watu mashuhuri wakiwa na fimbo za utawala na bakora.”
Kisha wakatoka jangwani kwenda Matana,
19kutoka Matana wakafika Nahalieli, kutoka Nahalieli wakafika Bamothi,
20na kutoka Bamothi wakafika kwenye bonde lililoko Moabu, mahali kilele cha Pisga kinatazamana na nyika.
21Israeli akawatuma wajumbe kumwambia Sihoni mfalme wa Waamori:
23Lakini Sihoni hakumruhusu Israeli apite katika nchi yake. Alilikutanisha jeshi lake lote, wakaondoka kwenda jangwani ili kupigana na Israeli. Alipofika huko Yahazi, akapigana na Israeli.
24Hata hivyo, Israeli walimshinda kwa upanga na kuimiliki nchi yake kutoka Mto Arnoni hadi Mto Yaboki, lakini ni kufikia nchi ya Waamoni tu, kwa sababu mipaka yake ilikuwa imezungushwa ukuta.
25Israeli wakaiteka miji yote ya Waamori na kuimiliki, pamoja na Heshboni na makazi yote yanayoizunguka.
26Heshboni ulikuwa mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa amepigana dhidi ya mfalme wa Moabu aliyetangulia, na akawa amechukua ardhi yake yote hadi Mto Arnoni.
27Ndiyo sababu watunga mashairi husema:
“Njoo Heshboni na ujengwe tena;
mji wa Sihoni na ufanywe upya.
28“Moto uliwaka kutoka Heshboni,
mwali wa moto kutoka mji wa Sihoni.
Uliteketeza Ari ya Moabu,
raia wa mahali pa Arnoni palipoinuka.
29Ole wako, ee Moabu!
Umeharibiwa, enyi watu wa Kemoshi!
Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi,
na binti zake kama mateka
kwa Mfalme Sihoni wa Waamori.
30“Lakini tumewashinda;
Heshboni umeharibiwa hadi Diboni.
Tumebomoa hadi kufikia Nofa,
ulioenea hadi Medeba.”
31Kwa hiyo Israeli akaishi katika nchi ya Waamori.
32Baada ya Musa kutuma wapelelezi kwenda mji wa Yazeri, Waisraeli waliteka makazi ya mji huo, na kuwafukuza Waamori walioishi huko.
33Kisha wakageuka na kwenda katika njia inayoelekea Bashani, naye Ogu mfalme wa Bashani pamoja na jeshi lake lote wakatoka kupigana nao huko Edrei.
34Bwana akamwambia Musa, “Usimwogope Ogu, kwa sababu nimeshamkabidhi mikononi mwako, pamoja na jeshi lake lote na nchi yake. Mtendee kama ulivyomtendea Sihoni mfalme wa Waamori, ambaye alitawala huko Heshboni.”
35Kwa hiyo wakamuua, pamoja na wanawe na jeshi lake lote, bila ya kumwacha hata mtu mmoja hai. Nao wakaimiliki nchi yake.