Zaburi 106

Zaburi 106

Zaburi 106

Wema wa Mwenyezi Mungu kwa watu wake

1Msifuni Mwenyezi Mungu.[#106:1 kwa Kiebrania ni Hallelu Yah ; pia 106:48.]

Mshukuruni Mwenyezi Mungu, kwa kuwa ni mwema;

fadhili zake zadumu milele.

2Ni nani awezaye kusimulia matendo makuu ya Mwenyezi Mungu

au kutangaza kikamilifu sifa zake?

3Heri wale wanaodumisha haki,

ambao daima wanafanya yaliyo mema.

4Ee Mwenyezi Mungu, unikumbuke unapowatendea mema watu wako,

uwe msaada wangu unapowaokoa,

5ili niweze kufurahia mafanikio ya wateule wako,

niweze kushiriki katika furaha ya taifa lako,

na kuungana na urithi wako katika kukusifu.

6Tumetenda dhambi, kama vile baba zetu walivyotenda,

tumekosa na tumetenda uovu.

7Baba zetu walipokuwa Misri,

hawakuzingatia maajabu yako,

wala hawakukumbuka wingi wa fadhili zako,

bali waliasi kando ya bahari,

ile Bahari ya Shamu.

8Hata hivyo aliwaokoa kwa ajili ya jina lake,

ili apate kudhihirisha uweza wake mkuu.

9Alikemea Bahari ya Shamu, nayo ikakauka,

akawaongoza katika vilindi vyake kama vile jangwani.

10Aliwaokoa mikononi mwa adui;

kutoka mikononi mwa adui aliwakomboa.

11Maji yaliwafunika adui zao,

hakunusurika hata mmoja.

12Ndipo walipoamini ahadi zake,

nao wakaimba sifa zake.

13Lakini walisahau upesi aliyowatendea,

wala hawakungojea ushauri wake.

14Jangwani walitawaliwa na tamaa zao,

walimjaribu Mungu nyikani.

15Kwa hiyo aliwapa kile walichoomba,

lakini akatuma juu yao ugonjwa wa kudhoofisha.

16Kambini walimwonea wivu Musa,

na pia Haruni aliyekuwa amewekwa wakfu kwa Mwenyezi Mungu.

17Ardhi ilifunguka ikawameza Dathani,

ikawazika Abiramu na kundi lake.

18Moto uliwaka katikati ya wafuasi wao,

mwali wa moto uliwateketeza waovu.

19Huko Horebu walitengeneza ndama,

na kuabudu sanamu ya kusubu kwa chuma.

20Waliubadilisha Utukufu wao

kwa sanamu ya fahali, ambaye hula majani.

21Walimsahau Mungu aliyewaokoa,

aliyetenda mambo makuu huko Misri,

22miujiza katika nchi ya Hamu

na mambo ya kutisha huko Bahari ya Shamu.

23Kwa hiyo alisema kwamba angewaangamiza:

kama Musa mteule wake,

asingesimama kati yao na Mungu

kuizuia ghadhabu yake kuwaangamiza.

24Kisha waliidharau ile nchi nzuri,

hawakuiamini ahadi yake.

25Walinung’unika ndani ya mahema yao,

wala hawakumtii Mwenyezi Mungu.

26Kwa hiyo akaapa kwa mkono ulioinuliwa

kwamba atawafanya waanguke jangwani,

27kuwatawanya wazao wao waanguke miongoni mwa mataifa,

na kuwatawanya katika nchi zote.

28Walijifunga nira na Baali wa Peori,

wakala dhabihu zilizotolewa kwa miungu isiyo na uhai.

29Waliichochea hasira ya Mwenyezi Mungu,

wakamkasirisha kwa matendo yao maovu,

nayo tauni ikazuka katikati yao.

30Lakini Finehasi alisimama na kuingilia kati,

nayo tauni ikazuiliwa.

31Hili likahesabiwa kwake haki,

kwa vizazi visivyo na mwisho vijavyo.

32Kwenye maji ya Meriba, walimkasirisha Mwenyezi Mungu,

janga likampata Musa kwa sababu yao;

33kwa maana walimwasi Roho wa Mungu,

na maneno yasiyofaa yakatoka mdomoni kwa Musa.

34Hawakuyaangamiza yale mataifa

kama Mwenyezi Mungu alivyowaagiza,

35bali walijichanganya na mataifa

na wakazikubali desturi zao.

36Waliabudu sanamu zao,

zikawa mtego kwao.

37Wakawatoa wana wao

na binti zao dhabihu kwa mashetani.

38Walimwaga damu isiyo na hatia,

damu za wana wao wa kiume na wa kike,

ambao waliwatoa dhabihu kwa sanamu za Kanaani,

nayo nchi ikanajisika kwa damu zao.

39Wakajinajisi wenyewe kwa yale waliyotenda;

kwa matendo yao wenyewe wakajifanyia ukahaba.

40Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawakasirikia watu wake

na akauchukia sana urithi wake.

41Akawakabidhi kwa mataifa

na adui zao wakawatawala.

42Adui zao wakawadhulumu

na kuwatia chini ya mkono wao.

43Mara nyingi aliwaokoa

lakini walizama kwenye uasi,

na wakajiharibu katika dhambi zao.

44Lakini akaangalia mateso yao

aliposikia kilio chao;

45kwa ajili yao akakumbuka agano lake,

na kutokana na upendo wake mkuu akapooza hasira yake.

46Akawafanya wahurumiwe

na wote waliowashikilia mateka.

47Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, tuokoe.

Tukusanye tena kutoka kwa mataifa,

ili tuweze kulishukuru jina lako takatifu,

na kushangilia katika sifa zako.

48Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli,

tangu milele na hata milele.

Watu wote na waseme, “Amen!”

Msifuni Mwenyezi Mungu.

Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™ Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Scriptures™ Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.