The chat will start when you send the first message.
1Bwana tusaidie, kwa kuwa wacha Mungu wametoweka;
waaminifu wametoweka miongoni mwa wanadamu.
2Kila mmoja humwambia jirani yake uongo;
midomo yao ya hila huzungumza kwa udanganyifu.
3Bwana na akatilie mbali midomo yote ya hila
na kila ulimi uliojaa majivuno,
4ule unaosema, “Kwa ndimi zetu tutashinda;
midomo ni mali yetu, bwana wetu ni nani?”
5“Kwa sababu wanyonge wanaonewa,
na wahitaji wanalia kwa uchungu,
nitainuka sasa,” asema Bwana .
“Nitawalinda kutokana na wale
wenye nia mbaya juu yao.”
6Maneno ya Bwana ni safi,
kama fedha iliyosafishwa katika tanuru,
iliyosafishwa mara saba.
7Ee Bwana , utatuweka salama
na kutulinda na kizazi hiki milele.
8Watu waovu huenda wakiringa kila mahali
wakati yule aliye mbaya sana
ndiye anayeheshimiwa miongoni mwa watu.