The chat will start when you send the first message.
1Nilimngoja Bwana kwa saburi,
naye akanijia na kusikia kilio changu.
2Akanipandisha kutoka shimo la uharibifu,
kutoka matope na utelezi;
akaiweka miguu yangu juu ya mwamba
na kunipa mahali imara pa kusimama.
3Akaweka wimbo mpya kinywani mwangu,
wimbo wa sifa kwa Mungu wetu.
Wengi wataona na kuogopa
na kuweka tumaini lao kwa Bwana .
4Heri mtu yule amfanyaye Bwana kuwa tumaini lake,
asiyewategemea wenye kiburi,
wale wenye kugeukia miungu ya uongo.
5Ee Bwana Mungu wangu,
umefanya mambo mengi ya ajabu.
Mambo uliyopanga kwa ajili yetu
hakuna awezaye kukuhesabia;
kama ningesema na kuyaelezea,
yangekuwa mengi mno kuyatangaza.
6Dhabihu na sadaka hukuvitaka,
lakini umefungua masikio yangu;
sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi
hukuzihitaji.
7Ndipo niliposema, “Mimi hapa, nimekuja:
imeandikwa kunihusu katika kitabu.
8Ee Mungu wangu,
natamani kuyafanya mapenzi yako;
sheria yako iko ndani ya moyo wangu.”
9Nimehubiri haki katika kusanyiko kubwa,
sikufunga mdomo wangu,
Ee Bwana , kama ujuavyo.
10Sikuficha haki yako moyoni mwangu;
ninasema juu ya uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha upendo wako na kweli yako
mbele ya kusanyiko kubwa.
11Ee Bwana , usinizuilie huruma zako,
upendo wako na kweli yako daima vinilinde.
12Kwa maana taabu zisizohesabika zimenizunguka,
dhambi zangu zimenikamata, hata nisiweze kuona.
Zimekuwa nyingi kuliko nywele za kichwa changu,
nao moyo unazimia ndani yangu.
13Ee Bwana , uwe radhi kuniokoa;
Ee Bwana , njoo hima unisaidie.
14Wote wanaotafuta kuniua,
waaibishwe na kufadhaishwa;
wote wanaotamani kuangamizwa kwangu,
wafukuzwe mbali kwa aibu.
15Wale wanaoniambia, “Aha! Aha!”
wafadhaishwe na iwe aibu yao.
16Lakini wote wanaokutafuta
washangilie na kukufurahia,
wale wanaoupenda wokovu wako siku zote waseme,
“Bwana atukuzwe!”
17Lakini mimi bado ni maskini na mhitaji;
Bwana na anifikirie.
Wewe ndiwe msaada wangu na Mwokozi wangu;
Ee Mungu wangu, usikawie.