Zaburi 45

Zaburi 45

Zaburi 45

Wimbo wa arusi ya kifalme

1Moyo wangu umesisimuliwa na jambo jema

ninapomsimulia mfalme mabeti yangu;

ulimi wangu ni kalamu ya mwandishi stadi.

2Wewe ni bora kuliko watu wengine wote

na midomo yako imepakwa neema,

kwa kuwa Mungu amekubariki milele.

3Jifunge upanga wako pajani mwako, ee mwenye nguvu,

jivike fahari na utukufu.

4Katika fahari yako, songa mbele kwa ushindi,

kwa ajili ya kweli, unyenyekevu na haki,

mkono wako wa kuume na uoneshe matendo ya kutisha.

5Mishale yako mikali na ichome mioyo ya adui za mfalme,

mataifa na yaanguke chini ya nyayo zako.

6Ee Mungu, kiti chako cha enzi

kitadumu milele na milele,

fimbo ya utawala wa haki

itakuwa fimbo ya utawala wa ufalme wako.

7Unaipenda haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako,

kwa kukupaka mafuta ya furaha.

8Mavazi yako yote yana harufu nzuri

ya manemane, udi na mdalasini;

kutoka majumba ya kifalme

yaliyopambwa kwa pembe za ndovu,

sauti za vinanda vya nyuzi

zinakufanya ufurahi.

9Binti za wafalme ni miongoni mwa wanawake wako waheshimiwa;

kuume kwako yupo bibi arusi malkia aliyevaa dhahabu ya Ofiri.

10Sikiliza, ewe binti, fikiri na utege sikio:

Sahau watu wako na nyumba ya baba yako.

11Mfalme ameshangazwa na uzuri wako;

mheshimu, kwa kuwa yeye ni bwana wako.

12Binti Tiro atakuletea zawadi,

watu wenye utajiri watatafuta upendeleo wako.

13Ufahari wote una binti mfalme katika chumba chake;

vazi lake limefumwa kwa nyuzi za dhahabu.

14Anaongozwa kwa mfalme,

akiwa amevalia mavazi yaliyotariziwa,

mabikira wenzake wanamfuata

na wanaletwa kwako.

15Wanaingizwa ndani kwa shangwe na furaha,

na kuingia katika jumba la mfalme.

16Wana wenu watachukua nafasi za baba zenu,

mtawafanya wakuu katika nchi yote.

17Nitadumisha kumbukumbu lako katika vizazi vyote,

kwa hiyo mataifa watakusifu milele na milele.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.