Zaburi 50

Zaburi 50

Zaburi 50

Ibada ya kweli

1Mwenye Nguvu, Mungu, Bwana ,

asema na kuiita dunia,

tangu mawio ya jua

hadi mahali pake liendapo kutua.

2Kutoka Sayuni, penye uzuri mkamilifu,

Mungu anaangaza.

3Mungu wetu anakuja na hatakaa kimya,

moto uteketezao unamtangulia,

akiwa amezungukwa na tufani kali.

4Anaziita mbingu zilizo juu,

na nchi, ili aweze kuwahukumu watu wake:

5“Nikusanyieni watu wangu waliowekwa wakfu,

waliofanya agano nami kwa dhabihu.”

6Nazo mbingu zinatangaza haki yake,

kwa maana Mungu mwenyewe ni hakimu.

7“Sikieni, enyi watu wangu, nami nitasema,

ee Israeli, nami nitashuhudia dhidi yenu:

Mimi ndimi Mungu, Mungu wenu.

8Sikukemei kwa sababu ya dhabihu zako,

au sadaka zako za kuteketezwa,

ambazo daima ziko mbele zangu.

9Sina haja na fahali wa banda lako,

au mbuzi wa zizi lako.

10Kwa maana kila mnyama wa msituni ni wangu,

na pia makundi ya mifugo juu ya vilima elfu.

11Ninamjua kila ndege mlimani,

nao viumbe wa kondeni ni wangu.

12Kama ningekuwa na njaa, nisingewaambia ninyi,

kwa maana ulimwengu ni wangu,

na vyote vilivyomo.

13Je, mimi hula nyama ya mafahali

au kunywa damu ya mbuzi?

14Toa sadaka za shukrani kwa Mungu,

timiza nadhiri zako kwake Yeye Aliye Juu Sana,

15na uniite siku ya taabu;

nami nitakuokoa, nawe utanitukuza.”

16Lakini kwake mtu mwovu, Mungu asema:

“Una haki gani kunena sheria zangu

au kuchukua agano langu mdomoni mwako?

17Unachukia mafundisho yangu

na kuyatupilia mbali maneno yangu.

18Unapomwona mwizi, unaungana naye,

unapiga kura yako pamoja na wazinzi.

19Unakitumia kinywa chako kunena maovu,

na kuuongoza ulimi wako kwa hila.

20Unamsengenya ndugu yako bila kukoma,

na kumsingizia mwana wa mama yako.

21Mambo haya unayafanya, nami nimekaa kimya,

ukadhani Mimi ni kama wewe kabisa.

Lakini nitakukemea

na kuweka mashtaka mbele yako.

22“Yatafakarini haya, ninyi mnaomsahau Mungu,

ama sivyo nitawararua vipande vipande,

wala hapatakuwa na yeyote wa kuwaokoa:

23Atoaye dhabihu za shukrani ananiheshimu mimi,

naye aiandaa njia yake

ili nimwoneshe wokovu wa Mungu.”

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.