Zaburi 69

Zaburi 69

Zaburi 69

Kilio cha kuomba msaada wakati wa dhiki

1Ee Mungu, niokoe,

kwa maana maji yamenifika shingoni.

2Ninazama kwenye vilindi vya matope,

pasipo mahali pa kukanyaga,

Nimefika kwenye maji makuu,

mafuriko yamenigharikisha.

3Nimechoka kwa kuomba msaada,

koo langu limekauka.

Macho yangu yanafifia,

nikimtafuta Mungu wangu.

4Wale wanaonichukia bila sababu

ni wengi kuliko nywele za kichwa changu;

wengi ni adui kwangu bila sababu,

wale wanaotafuta kuniangamiza.

Ninalazimishwa kurudisha

kitu ambacho sikuiba.

5Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu,

wala hatia yangu haikufichika kwako.

6Ee Bwana, Bwana wa majeshi,

wanaokutumaini wasiaibishwe

kwa ajili yangu;

wanaokutafuta wasifedheheshwe kwa ajili yangu,

Ee Mungu wa Israeli.

7Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako,

aibu imefunika uso wangu.

8Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,

mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe.

9Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila,

matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.

10Ninapolia na kufunga,

lazima nivumilie matusi.

11Ninapovaa gunia,

watu hunidharau.

12Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga,

nimekuwa wimbo wa walevi.

13Lakini Ee Bwana , ninakuomba,

kwa wakati ukupendezao;

katika upendo wako mkuu, Ee Mungu,

unijibu kwa wokovu wako wa hakika.

14Uniokoe katika matope,

usiniache nizame;

niokoe na hao wanaonichukia,

kutoka kwa vilindi vya maji.

15Usiache mafuriko yanigharikishe

au vilindi vinimeze,

au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu.

16Ee Bwana , unijibu, kwa wema wa upendo wako;

kwa huruma zako nyingi unigeukie.

17Usimfiche mtumishi wako uso wako,

uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.

18Njoo karibu uniokoe,

nikomboe kwa sababu ya adui zangu.

19Unajua jinsi ninavyodharauliwa,

kufedheheshwa na kuaibishwa,

adui zangu wote unawajua.

20Dharau zimenivunja moyo

na nimekata tamaa,

nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata,

wa kunituliza, lakini sikumpata.

21Waliweka nyongo katika chakula changu

na walinipa siki nilipokuwa na kiu.

22Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego,

nayo iwe upatilizo na tanzi.

23Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona,

nayo migongo yao iinamishwe daima.

24Uwamwagie ghadhabu yako,

hasira yako kali na iwapate.

25Mahali pao na pawe ukiwa,

wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao.

26Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi,

na kuzungumza kuhusu maumivu ya wale uliowaumiza.

27Walipize uovu juu ya uovu,

usiwaache washiriki katika wokovu wako.

28Wafutwe kutoka kitabu cha uzima

na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.

29Lakini mimi niko katika maumivu na dhiki;

Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.

30Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,

nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.

31Hili litampendeza Bwana kuliko ngʼombe dume,

zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.

32Maskini wataona na kufurahi:

ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!

33Bwana huwasikia wahitaji

wala hadharau watu wake waliotekwa.

34Mbingu na dunia zimsifu,

bahari na vyote viendavyo ndani yake,

35kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni

na kuijenga tena miji ya Yuda.

Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki,

36watoto wa watumishi wake watairithi

na wale wote wanaolipenda jina lake

wataishi humo.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.