The chat will start when you send the first message.
1Ee Bwana , Mungu wangu, ninakukimbilia wewe,
uniokoe na kunikomboa na wote wanaonifuatia,
2la sivyo watanirarua kama simba
na kunichana vipande vipande, asiwepo wa kuniokoa.
3Ee Bwana , Mungu wangu, kama nimetenda haya
na kuna hatia mikononi mwangu,
4au ikiwa nimemtenda uovu aliye na amani nami,
au nimemnyangʼanya adui yangu pasipo sababu,
5basi adui anifuatie na kunipata,
auponde uhai wangu ardhini
na kunilaza mavumbini.
6Amka kwa hasira yako, Ee Bwana ,
inuka dhidi ya ghadhabu ya adui zangu.
Amka, Mungu wangu, uamue haki.
7Kusanyiko la watu na likuzunguke.
Watawale kutoka juu.
8Bwana na awahukumu makabila ya watu.
Nihukumu Ee Bwana ,
kwa kadiri ya haki yangu,
kwa kadiri ya uadilifu wangu,
Ewe Uliye Juu Sana.
9Ee Mungu mwenye haki,
uchunguzaye mawazo na mioyo,
komesha ghasia za waovu
na ufanye wenye haki waishi kwa amani.
10Ngao yangu ni Mungu Aliye Juu Sana,
anayewaokoa wanyofu wa moyo.
11Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
Mungu anayeghadhibika kila siku.
12Mtu asipotubu,
Mungu ataunoa upanga wake,
ataupinda na kuufunga uzi upinde wake.
13Ameandaa silaha zake kali,
ameweka tayari mishale yake ya moto.
14Yeye aliye na mimba ya uovu
na anayechukua mimba ya ghasia huzaa uongo.
15Yeye anayechimba shimo na kulifukua
hutumbukia katika shimo alilochimba mwenyewe.
16Ghasia anazozianzisha humrudia mwenyewe,
ukatili wake humrudia kichwani.
17Nitamshukuru Bwana kwa ajili ya haki yake,
na nitaliimbia sifa jina la Bwana Aliye Juu Sana.