The chat will start when you send the first message.
1Ee Mchungaji wa Israeli tusikie,
wewe umwongozaye Yusufu kama kundi;
wewe uketiye kwenye kiti cha enzi
katikati ya makerubi, angaza
2mbele ya Efraimu, Benyamini na Manase.
Uamshe nguvu zako,
uje utuokoe.
3Ee Mungu, uturejeshe,
utuangazie uso wako,
ili tuweze kuokolewa.
4Ee Bwana Mungu wa majeshi,
hata lini hasira yako itawaka
dhidi ya maombi ya watu wako?
5Umewalisha kwa mkate wa machozi,
umewafanya wanywe machozi bakuli tele.
6Tumekuwa chanzo cha ugomvi kwa majirani zetu,
na adui zetu wanatudhihaki.
7Ee Mungu wa majeshi, uturejeshe;
utuangazie uso wako,
nasi tuweze kuokolewa.
8Ulileta mzabibu kutoka Misri,
ukawafukuza mataifa, ukaupanda.
9Uliandaa shamba kwa ajili yake,
mizizi ikawa imara, ukajaza nchi.
10Milima ilifunikwa kwa kivuli chake,
matawi yake yakafunika mierezi mikubwa.
11Matawi yake yalienea hadi Baharini,[#80:11 pengine ni Bahari ya Mediterania]
machipukizi yake hadi kwenye Mto.
12Mbona umebomoa kuta zake
ili wote wapitao karibu
wazichume zabibu zake?
13Nguruwe mwitu wanauharibu,
na viumbe wa kondeni hujilisha humo.
14Turudie, Ee Mungu wa majeshi!
Tazama chini kutoka mbinguni na uone!
Linda mzabibu huu,
15mche ulioupanda kwa mkono wako wa kuume,
mwana uliyemlea
kwa ajili yako mwenyewe.
16Mzabibu wako umekatwa, umechomwa moto,
unapowakemea, watu wako huangamia.
17Mkono wako na utulie juu ya mtu aliye katika mkono wako wa kuume,
mwana wa mtu uliyemlea kwa ajili yako mwenyewe.
18Ndipo hatutakuacha tena,
utuhuishe, nasi tutaliitia jina lako.
19Ee Bwana Mungu wa majeshi, uturejeshe;
utuangazie uso wako,
ili tuweze kuokolewa.