Zaburi 85

Zaburi 85

Zaburi 85

Maombi kwa ajili ya ustawi wa taifa

1Ee Bwana , ulionesha wema kwa nchi yako.

Ulimrejeshea Yakobo baraka zake.

2Ulisamehe uovu wa watu wako,

na kufunika dhambi zao zote.

3Uliweka kando ghadhabu yako yote

na umegeuka na kuiacha hasira yako kali.

4Ee Mungu Mwokozi wetu, uturejeshe tena,

nawe uiondoe chuki yako juu yetu.

5Je, utatukasirikia milele?

Utaendeleza hasira yako kwa vizazi vyote?

6Je, hutatuhuisha tena,

ili watu wako wakufurahie?

7Utuoneshe upendo wako usiokoma, Ee Bwana ,

utupe wokovu wako.

8Nitasikiliza lile atakalosema Mungu aliye Bwana ;

anaahidi amani kwa watu wake, watakatifu wake:

lakini nao wasirudie upumbavu.

9Hakika wokovu wake uko karibu na wale wamchao,

ili utukufu wake udumu katika nchi yetu.

10Upendo na uaminifu hukutana pamoja,

haki na amani hubusiana.

11Uaminifu huchipua kutoka nchi,

haki hutazama chini kutoka mbinguni.

12Naam, hakika Bwana atatoa kilicho chema,

nayo nchi yetu itazaa mavuno yake.

13Haki itatangulia mbele yake

na kutengeneza njia kwa ajili ya hatua zake.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.