Zaburi 88

Zaburi 88

Zaburi 88

Kilio kwa ajili ya kuomba msaada

1Ee Bwana , Mungu uniokoaye,

nimelia mbele zako usiku na mchana.

2Maombi yangu yafike mbele zako,

utegee kilio changu sikio lako.

3Kwa maana nafsi yangu imejaa taabu,

na maisha yangu yanakaribia kaburi.

4Nimehesabiwa miongoni mwa wale wanaoshuka shimoni;

niko kama mtu asiye na nguvu.

5Nimetengwa pamoja na wafu,

kama waliochinjwa walalao kaburini,

ambao huwakumbuki tena,

ambao wamekatiliwa mbali na uangalizi wako.

6Umenitupa katika shimo lenye kina kirefu sana,

katika vina vya giza nene.

7Ghadhabu yako imekuwa nzito juu yangu,

umenigharikisha kwa mawimbi yako yote.

8Umenitenga na rafiki zangu wa karibu

na kunifanya chukizo kwao.

Nimezuiliwa, wala siwezi kutoroka;

9nuru ya macho yangu

imefifia kwa ajili ya huzuni.

Ee Bwana , ninakuita kila siku,

ninakunyooshea wewe mikono yangu.

10Je, wewe huwaonesha wafu maajabu yako?

Je, wale waliokufa huinuka na kukusifu?

11Je, upendo wako hutangazwa kaburini,

uaminifu wako katika Uharibifu?

12Je, maajabu yako hujulikana mahali pa giza,

au matendo yako ya haki katika nchi ya usahaulifu?

13Lakini ninakulilia wewe, Ee Bwana , unisaidie;

asubuhi maombi yangu huja mbele zako.

14Ee Bwana , kwa nini unanikataa

na kunificha uso wako?

15Tangu ujana wangu nimeteseka, nikakaribia kifo;

nimepatwa na mapigo yako, nami nimekata tamaa.

16Ghadhabu yako imepita juu yangu;

mapigo yako yameniangamiza.

17Mchana kutwa zinanizunguka kama mafuriko;

zimenimeza kabisa.

18Umeniondolea rafiki na wapendwa wangu;

giza limekuwa rafiki yangu wa karibu kuliko wote.

Neno: Biblia Takatifu™ Neno™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 na Biblica, Inc. Imetumiwa kwa ruhusa. Haki zote zimehifadhiwa duniani kote. Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015, 2025 by Biblica, Inc. Used with permission. All rights reserved worldwide.
Published by: Biblica, Inc.