The chat will start when you send the first message.
1Mwimbieni Bwana wimbo mpya;
mwimbieni Bwana dunia yote.
2Mwimbieni Bwana , lisifuni jina lake;
tangazeni wokovu wake siku baada ya siku.
3Tangazeni utukufu wake katika mataifa,
matendo yake ya ajabu miongoni mwa mataifa yote.
4Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kustahili kusifiwa kuliko wote;
yeye ni wa kuogopwa kuliko miungu yote.
5Kwa maana miungu yote ya mataifa ni sanamu,
lakini Bwana aliziumba mbingu.
6Fahari na enzi viko mbele yake;
nguvu na utukufu vimo patakatifu pake.
7Mpeni Bwana , enyi jamaa za mataifa,
mpeni Bwana utukufu na nguvu.
8Mpeni Bwana utukufu unaostahili jina lake;
leteni sadaka na mje katika nyua zake.
9Mwabuduni Bwana katika uzuri wa utakatifu wake;
dunia yote na itetemeke mbele zake.
10Semeni katika mataifa kwamba, “Bwana anatawala.”
Ulimwengu ameuweka imara, hauwezi kusogezwa;
atawahukumu watu kwa uadilifu.
11Mbingu na zishangilie, nchi na ifurahi;
bahari na ivume, na vyote vilivyo ndani yake;
12mashamba na yashangilie,
pamoja na vyote vilivyomo.
Kisha miti yote ya msituni itaimba kwa furaha;
13itaimba mbele za Bwana kwa maana anakuja,
anakuja kuihukumu dunia.
Ataihukumu dunia kwa haki,
na mataifa katika kweli yake.