The chat will start when you send the first message.
1Ee Yerusalemu, vua nguo za matanga na huzuni,[#Isa 52:1; 61:3,10; Ufu 21:2]
Uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu milele.
2Jifunge nguo ya haki itokayo kwa Mungu,
Jipige kilemba kichwani cha utukufu wake Aliye wa Milele.
3Maana Mungu ataidhihirisha nuru yako duniani kote,
4Na jina lako litaitwa na Mungu daima,
Amani ya haki, na Utukufu wa utauwa.
5Ondoka, Ee Yerusalemu, usimame juu;
Tazama upande wa mashariki, uangalie.
Toka machweo ya jua hata mawio yake wanao wanakusanyika
Kwa neno lake Yeye Aliye Mtakatifu,
Wakifurahi kwa kuwa Mungu amewakumbuka.
6Waliondoka kwako kwa miguu, wakikokotwa na adui zao,
Lakini Mungu anawarejeza kwako wameinuliwa juu kwa heshima
Kama katika kiti cha enzi.
7Maana kwa maagizo ya Mungu
Kila kilima kirefu kitashushwa,
Na milima ya milele.
Na mabonde yote yatajazwa,
Hata nchi iwe sawa,
Ili Israeli aende salama
Katika utukufu wa Mungu.
8Nayo misitu, na miti yote itoayo harufu nzuri,
Imemtia Israeli kivuli kwa amri ya Mungu;
9Kwa kuwa Mungu atamwongoza Israeli kwa furaha
Katika mwangaza wa utukufu wake,
Kwa ile rehema na haki itokayo kwake.