Ezra 4

Ezra 4

Ujenzi wa hekalu wapingwa

1Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, hekalu,

2wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa koo za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi tumemtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa.[#Est 8:17; 2 Fal 17:24,32,33]

3Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa koo za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru.[#Yn 4:9; Mdo 8:21; 2 Nya 36:22,23; Ezr 6:3; Isa 44:28]

4Ndipo wakazi wa nchi wakawavunja moyo watu wa Yuda, wakawafanya wawe na hofu ya kujenga.[#Ezr 3:3; Isa 35:3,4; Yer 38:4]

5Wakawahonga maofisa, ili kuwakatisha tamaa katika mpango wao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.

Ujenzi wa Yerusalemu wapingwa

6Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu.

7Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na wenzao wengine, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kusomwa kwa lugha ya Kiaramu.

8Nao Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi;[#Zab 112:6; Zek 1:14; Rum 8:28]

9Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami;[#2 Fal 17:30,31]

10na watu wengine wa mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng'ambo ya Mto; na kadhalika.[#Ezr 7:12]

11Hii ndiyo nakala ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta;

Watumishi wako, watu walio ng'ambo ya Mto; nakadhalika.

12Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake.[#Amo 7:10; Lk 23:2; Mdo 24:5]

13Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara.[#Ezr 7:24; Mt 9:9]

14Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme.

15Ili habari zichunguzwe katika kitabu cha kumbukumbu za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha kumbukumbu ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na wakuu wa mikoa, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa.[#Est 3:8; Mdo 17:6,7]

16Tunamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, basi utakuwa huna milki katika sehemu ya nchi iliyo ng'ambo ya mto.

17Ndipo mfalme akatuma majibu;

Kwa Rehumu, mtawala, na Shimshai, mwandishi, na wenzao wengine waliokaa katika Samaria, na penginepo ng'ambo ya Mto, Salamu; na kadhalika.

18Ule waraka mliotutumia umesomwa wazi mbele yangu, nami nikauelewa.

19Nikatoa amri, na watu wametafuta habari; ikaonekana ya kuwa mji huu zamani umewaasi wafalme, na ya kuwa uasi na fitina zimefanyika ndani yake.

20Tena walikuwako wafalme wakuu juu ya Yerusalemu, waliotawala nchi yote iliyo ng'ambo ya Mto; wakapewa kodi, na ada, na ushuru.[#1 Nya 18:3; Zab 72:8; Mwa 15:18]

21Sasa toeni amri kuwakomesha watu hawa kazi yao, mji huu usijengwe, hadi nitakapotoa amri.

22Tena jihadharini, msilegee katika jambo hili; kwa nini madhara yazidi, na wafalme wapate hasara?

23Kisha nakala ya barua hiyo ya mfalme Artashasta iliposomwa mbele ya Rehumu, mtawala na Shimshai, mwandishi, na wenzao, wakaenda Yerusalemu upesi, kwa Wayahudi, wakawakomesha kwa nguvu na kwa kuwashurutisha.[#Mit 4:16]

24Hivyo kazi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu ikakoma; nayo ikakoma hadi mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi.[#Ayu 20:5]

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania