Isaya 22

Isaya 22

Onyo la kuharibiwa kwa Yerusalemu

1Ufunuo juu ya bonde la maono.

Sasa una nini, wewe,

Hata umepanda pia juu ya madari ya nyumba?

2Ewe uliyejaa makelele,

Mji wa ghasia, mji wenye furaha;

Watu wako waliouawa hawakuuawa kwa upanga,

Wala hawakufa vitani.

3Wakuu wako wote wamekimbia pamoja,

Wamefungwa wasiutumie upinde.

Wote walioonekana wamefungwa pamoja,

Wamekimbia mbali sana.

4Kwa sababu hiyo nasema, Geuza uso wako usinitazame, nipate kulia kwa uchungu; usijishughulishe kunifariji, kwa ajili ya kuharibika kwake binti ya watu wangu.

5Kwa maana siku ya kutaabika, siku ya kukanyagwa, siku ya fujo inakuja, itokayo kwa Bwana, BWANA wa majeshi, katika bonde la Maono; inabomoa kuta; na kuililia milima.[#Est 3:15; Omb 1:5]

6Na Elamu wameshika podo, pamoja na magari ya vita, na watu wenye kupanda farasi; na Kiri wameifunua ngao.[#Isa 21:2; Yer 49:35]

7Hata ikawa mabonde yako mateule yamejaa magari ya vita, nao wapandao farasi wamejipanga katika malango.

8Kisha alikiondoa kifuniko cha Yuda, nawe siku hiyo ulivitazama vyombo vya vita katika nyumba ya mwituni.[#1 Fal 7:2]

9Nanyi mlipaona mahali palipobomoka katika mji wa Daudi ya kuwa ni pengi, nanyi mliyakusanya maji ya birika la chini.[#2 Fal 20:20; 2 Nya 32:4; Wim 4:4]

10Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.

11Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani.[#Neh 3:16]

12Siku hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung'oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia;

13na kumbe! Furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng'ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.[#Isa 5:12; Amo 6:3; Lk 17:26-29; Isa 56:12; 1 Kor 15:32]

14Na yeye BWANA wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, BWANA wa majeshi.[#1 Sam 3:14; Eze 24:13]

Shutuma kwa maofisa wa kujipendekeza

15Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Haya! Nenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie,[#2 Fal 18:37; Isa 36:3; 1 Fal 4:6]

16Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali!

17Tazama, BWANA atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzongazonga.

18Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa huko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako.

19Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo.

20Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia;[#2 Fal 18:18]

21nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda.[#Ayu 29:16]

22Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.[#Ufu 3:7]

23Nami nitamkaza kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake.[#Ezr 9:8]

24Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia.

25Katika siku ile, asema BWANA wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana BWANA amesema haya.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania