Zaburi 63

Zaburi 63

Faraja na uhakikisho katika Bwana

1Ee MUNGU, Mungu wangu, nitakutafuta mapema,[#1 Sam 23:14]

Nafsi yangu inakuonea kiu,

Mwili wangu wakuonea shauku,

Katika nchi kame na uchovu, isiyo na maji.

2Ndivyo nilivyokutazama katika patakatifu,[#1 Nya 16:11]

Nizione nguvu zako na utukufu wako.

3Maana fadhili zako ni njema kuliko uhai;[#Yn 3:16]

Midomo yangu itakusifu.

4Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai;

Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu.

5Nafsi yangu itakinai kama kushiba mafuta na vinono;[#Zab 17:15; Isa 25:6]

Kinywa changu kitakusifu kwa midomo ya furaha.

6Ninapokukumbuka kitandani mwangu,[#Zab 149:5]

Ninakutafakari usiku kucha.

7Maana Wewe umekuwa msaada wangu,[#2 Kor 1:10]

Na uvulini mwa mbawa zako nitashangilia.

8Nafsi yangu inaambatana nawe sana;[#Isa 26:9]

Mkono wako wa kuume unanitegemeza.

9Bali waitafutao nafsi yangu, ili kuiangamiza,

Wataingia katika vilindi vya nchi.

10Watatolewa wafe kwa nguvu za upanga,

Watakuwa riziki za mbwamwitu.

11Bali mfalme atamfurahia Mungu,[#Sef 1:5]

Kila aapaye kwa Yeye atashangilia,

Kwa maana vinywa vya waongo vitafumbwa.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania