Zaburi 71

Zaburi 71

Sala ya ulinzi wa daima na msaada

1Nimekukimbilia Wewe, BWANA,

Nisiaibike milele.

2Kwa haki yako uniponye, uniponye,

Unitegee sikio lako, uniokoe.

3Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu,[#Zab 44:4]

Ngome imara ya wokovu wangu.

Maana wewe,

Ndiwe mwamba wangu na ngome yangu.

4Ee Mungu wangu, uniponye mkononi mwa mkorofi,

Katika mkono wake mwovu na mdhalimu,

5Maana ndiwe tegemeo langu, Ee Bwana MUNGU,[#Yer 17:7; Rum 15:13]

Tumaini langu tokea ujana wangu.

6Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa,[#Zab 22:9; Isa 46:3; Yer 3:4]

Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu,

Ninakusifu Wewe daima.

7Nimekuwa kioja kwa watu wengi,[#Isa 8:18; Zek 3:8; 1 Kor 4:9]

Lakini wewe ndiwe kimbilio langu la nguvu.

8Kinywa changu kitajazwa sifa zako,

Na heshima yako mchana kutwa.

9Usinitupe wakati wa uzee,

Nguvu zangu zipungukapo usiniache.

10Kwa maana adui zangu husema juu yangu,[#2 Sam 17:1; Mt 27:1]

Nao wanaotaka kuniua hushauriana.

11Wakisema, Mungu amemwacha,

Mfuatieni, mkamateni, hakuna wa kumponya.

12Ee Mungu, usiwe mbali nami;[#Zab 22:11; 35:22; 70:1]

Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia.

13Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu.[#Zab 35:4; 40:14]

Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya.

14Lakini mimi nitakutumainia daima,

Nitaendelea kukusifu zaidi na zaidi.

15Lakini mimi nitakutumainia daima[#Zab 35:28; 40:5]

Na nitaendelea kukusifu zaidi na zaidi.

16Nitakuja na mambo ya ajabu ya Bwana MUNGU;[#Zek 10:12; Efe 3:16; Flp 4:13; 2 Tim 2:1]

Nitawakumbusha watu haki yako Wewe peke yako.

17Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu;

Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.

18Na hata nikiwa ni mzee mwenye mvi,

Ee Mungu, usiniache.

Hata niwaeleze watu wa kizazi hiki nguvu zako,

Na kila atakayekuja uweza wako.

19Na haki yako, Ee Mungu,[#Zab 57:10; Mit 24:7; Isa 5:16; Kut 15:11; Zab 35:10; Isa 40:18,25]

Imefika juu sana.

Wewe uliyefanya mambo makuu;

Ee Mungu, ni nani aliye kama Wewe?

20Wewe, uliyetuonesha mateso mengi, mabaya,[#Zab 60:3; Hos 6:1]

Utatuhuisha tena.

Utatupandisha juu tena

Tokea pande za chini ya nchi.

21Laiti ungeniongezea ukuu!

Urejee tena na kunifariji moyo.

22Nami nitakushukuru kwa kinanda,[#2 Fal 19:22; Isa 60:9]

Na kweli yako, Ee Mungu wangu.

Nitakuimbia Wewe kwa kinubi,

Ee Mtakatifu wa Israeli.

23Midomo yangu itafurahi sana nikuimbiapo,[#Zab 103:4]

Na nafsi yangu uliyoikomboa.

24Ulimi wangu nao utasimulia

Haki yako mchana kutwa.

Kwa maana wameaibishwa,

Wametahayarika, wanaonitakia mabaya.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania