Yoshua Mwana wa Sira 2

Yoshua Mwana wa Sira 2

Wajibu kwa Mungu

1Mwanangu, ukija kumtumikia BWANA,

Weka tayari roho yako kwa kujaribiwa.

2Ujitengeneze moyo ustahimili, wala isitaharuki siku ya kuteswa.

3Uambatane naye wala usijitenge tena, ili mwisho wako ukuzwe.

4Kila utakalopelekewa ulipokee kwa kuchangamka moyo, uyavumilie mabadiliko ya unyonge wako.

5Maana dhahabu hujaribiwa motoni, na watu wateule kalibuni mwa unyonge.[#Mit 3:5-6; 1 Pet 1:7; #Mit 6:18; Yn 14:15,21,23]

6Basi umwamini Yeye, naye atakusaidia; ukazinyoshe njia zako, na kulikaza taraja lako katika Yeye.

7Enyi mnaomcha BWANA,

Zingojeeni rehema zake,

Msigeuke upande msije mkaanguka.

8Enyi mnaomcha BWANA,

Mwaminini Yeye sana,

Thawabu yenu haitawapotea.

9Enyi mnaomcha BWANA,

Sasa tarajieni mema,

Na furaha ya daima na rehema.

10Angalieni vizazi vya kale mkaone;

Nani aliyemtumaini BWANA akaaibika?

Nani aliyekaa hali ya kumcha akaachwa?

Nani aliyemwita akadharauliwa?

11Mradi BWANA yu mwenye huruma na rehema,

Husamehe dhambi na kuokoa wakati wa shida.

12Ole wao wenye mioyo ya woga,

Wenye mikono iliyolegea,

Wakosaji waendao njia mbili.

13Ole wake aliye dhaifu wa moyo,

Kwa maana amekosa imani,

Kwa hiyo hatahifadhika.

14Ole wenu ninyi nanyi,

Enyi mliopotewa na saburi,

Mtafanyaje BWANA atakapowajia?

15Wale wamchao BWANA

Hawatayaasi maneno yake;

Wampendao watazishika amri zake.

16Wale wamchao BWANA

Watatafuta mapenzi yake;

Nao wampendao watashiba torati.

17Wale wamchao BWANA

Watajitengeneza mioyo;

Na kunyenyekea machoni pake;

18Tutaanguka katika mikono ya BWANA,

Wala si katika mikono ya wanadamu;

Kwa maana kama ilivyo enzi yake,

Ndivyo zilivyo na rehema zake;

Na kama lilivyo jina lake,

Ndivyo yalivyo na matendo yake.

The Holy Bible in Kiswahili, Revised Union Version © Bible Society of Tanzania and Bible Society of Kenya, 2013. 
Published by: Bible Society of Tanzania