1 Wamakabayo 16

1 Wamakabayo 16

1Yohane, mwana wa Simoni, akaondoka Gazara, akaenda kumwarifu baba yake mambo aliyokuwa amefanya Kendebeo.

2Simoni akawaambia Yohane na Yuda, wanawe wakubwa, “Mimi na ndugu zangu, na familia yote ya baba yangu, tumepiga vita vya Israeli maisha yetu yote, na mara nyingi tumefanikiwa kuiokoa Israeli.

3Mimi sasa ni mzee, lakini nyinyi, shukrani kwa Mungu, mmejaa utomvu wa utu uzima. Lazima mchukue nafasi yangu na ile ya ndugu yangu katika kulipigania taifa letu. Bwana awe nanyi kuwasaidia.”

4Hapo Yohane akaunda jeshi la Kiisraeli la askari hodari na wapandafarasi 20,000, akaondoka kumkabili Kendebeo. Baada ya kulala Modeini,

5mapema asubuhi iliyofuata wakaelekea kwenye tambarare. Huko wakaona jeshi kubwa la askari wa miguu na wapandafarasi linakuja kupambana nao, lakini kati yao na maadui palikuwa na mto.

6Yohane na jeshi lake wakajipanga kivita dhidi ya maadui, na askari walipoonesha wanaogopa kuvuka mto, Yohane akatangulia kuvuka, na watu wake wakamfuata.

7Yohane akaligawa jeshi lake na kuwaweka wapandafarasi katikati ya askari wa miguu, kwa sababu idadi ya maadui wapandafarasi ilikuwa kubwa sana.

8Tarumbeta zilipigwa, mapambano yakaanza. Kendebeo na jeshi lake walipigwa vibaya sana, wakashindwa na kupoteza askari wengi. Walionusurika kifo wakakimbilia Kedroni, kwenye ngome yao.

9Yuda alikuwa amejeruhiwa vitani, lakini nduguye, Yohane, akaendelea kuwafuatia maadui hadi Kedroni, mji ambao Kendebeo alikuwa ameujenga upya.

10Askari hao waliokuwa wanatoroka walikimbilia kwenye minara iliyokuwa katika mashamba ya Ashdodi na Yohane akauchoma moto mji huo. Siku hiyo askari 2,000 wa maadui waliuawa; Yohane akarejea salama Yudea.

Kuuawa kwa Simoni na wanawe wawili

11Simoni, kuhani mkuu, alikuwa amemteua Tolemai, mwana wa Abubo, awe kamanda kwa ajili ya tambarare za Yeriko. Tolemai alikuwa tajiri sana,

12kwa sababu alikuwa mkwe wa Simoni.

13Lakini alikuwa na tamaa mno, akataka kuchukua utawala wa nchi. Hivi akafanya hila ya kumwua Simoni na wanawe.

14Simoni, pamoja na wanawe, Matathia na Yuda, alikuwa anatembelea miji mbalimbali, ili kuona mahitaji yao. Mwezi wa Shebati yaani wa kumi na moja, mwaka 177, wakawasili Yeriko.[#16:14 Ni sawa na 134 K.K.]

15Tolemai, akiwa bado anakula njama ya kumwua Simoni na wanawe, akawapokea katika ngome ndogo iliyoitwa Doki ambayo alikuwa ameijenga mwenyewe. Akawafanyia karamu kubwa, lakini alikuwa amewaficha watu humo ngomeni.

16Simoni na wanawe walipokuwa wamelewa, Tolemai na watu wake wakajitokeza na mapanga mikononi, wakaingia mbio katika ukumbi wa karamu, wakawaua Simoni na wanawe wawili, na baadhi ya wahudumu.

17Kwa tendo hilo ovu na la uhaini, Tolemai alikuwa amelipa jema kwa baya.

18Kisha Tolemai akaandika taarifa ya hayo aliyokuwa ametenda, akaipeleka kwa mfalme. Katika taarifa hiyo aliomba apelekewe askari wa kumsaidia, na kwamba apewe utawala wa miji na wa nchi yenyewe.

19Aliandika barua kwa maofisa wa jeshi akiwaalika wajiunge naye na kuwaahidia fedha, dhahabu, na zawadi maridhawa. Halafu akawatuma baadhi ya watu wake kwenda Gazara kumwua Yohane,

20na wengine kwenda kushika mji wa Yerusalemu na mlima wa hekalu.

21Lakini mtu mmoja akapiga mbio, akafika Gazara kabla watu hao wa Tolemai hawajafika, akamwarifu Yohane kwamba baba yake na ndugu zake walikuwa wameuawa, na kwamba Tolemai alikuwa amewatuma askari kumwua yeye Yohane.

22Yohane alifadhaika sana aliposikia hayo, lakini, kwa vile alikuwa ametahadharishwa kabla, alifaulu kuwakamata na kuwaulia mbali watu waliokuwa wametumwa kumuua yeye.

23Habari nyingine za Yohane: Kuhusu vita vyake, matendo yake ya ujasiri, ujenzi wake wa kuta, na mafanikio yake mengine,

24zote zimeandikwa katika kumbukumbu za utawala wake kama kuhani mkuu, tangu alipoupata baada ya baba yake.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania