Isaya 12

Isaya 12

Wimbo wa shukrani

1Siku hiyo mtasema:

“Nakushukuru, ee Mwenyezi-Mungu,

maana ingawa ulinikasirikia,

hasira yako imetulia,

nawe umenifariji.

2Mungu ndiye mwenye kuniokoa,[#Taz Kut 15:2; Zab 118:14]

nitamtegemea yeye, wala sitaogopa;

Mwenyezi-Mungu hunijalia nguvu;

yeye mwenyewe ndiye aniokoaye.”

3Mtachota maji kwa furaha

kutoka visima vya wokovu.

4Siku hiyo mtasema:

“Mshukuruni Mwenyezi-Mungu

mwombeni kwa jina lake.

Yajulisheni mataifa matendo yake,

tangazeni kuwa jina lake limetukuka.

5Mwimbieni Mwenyezi-Mungu sifa

kwa kuwa ametenda mambo makuu;

haya na yajulikane duniani kote.

6Pazeni sauti na kuimba kwa furaha,

enyi wakazi wa Siyoni,

maana aliye mkuu miongoni mwenu

ndiye Mungu, Mtakatifu wa Israeli.”

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania