Yudithi 5

Yudithi 5

Halmashauri ya vita kambini mwa Holoferne

1Holoferne, jenerali wa jeshi la Ashuru, aliposikia kuwa watu wa Israeli wamejitayarisha kwa vita kwa kufunga njia za milimani, wamejenga ngome milimani, na kuweka vizuizi vya barabarani mbugani,

2aliwaka hasira. Hivyo, aliwaita wakuu wa Wamoabu, makamanda wa Waamoni na magavana wote wa eneo la pwani ya bahari ya Mediteranea.

3Walipokusanyika, aliwaambia, “Nyinyi mnaokaa katika nchi hii ya Kanaani, hebu niambieni, ni watu wa namna gani wanaokaa katika milima hii? Wanakaa katika miji gani? Je, jeshi lao ni kubwa kiasi gani? Je, uwezo na nguvu zao vinatokana na nini? Je, ni nani mfalme anayelitawala na kuliongoza jeshi lao?

4Kwa nini wamekataa kujitokeza ili kunilaki kama watu wengine wa magharibi?”

Hotuba ya Akioro

5Ndipo Akioro, kiongozi wa Waamoni wote, alipomwambia Holoferne, “Bwana, nakuomba mimi mtumishi wako, usikilize ninalotaka kusema. Nitakueleza ukweli kuhusu watu wanaokaa kwenye milima karibu na wewe. Mimi mtumishi wako sitakuambia uongo wowote.

6Watu hao ni wazawa wa Wakaldayo.

7Hapo zamani walikaa katika nchi ya Mesopotamia. Lakini kwa sababu hawakuweza kuziabudu sanamu za miungu ya wazee wao huko Ukaldayo,

8wala hawakuzifuata njia zao, wakahama ili kumwabudu Mungu wa mbinguni. Mungu waliyejifunza kumkiri. Walipofukuzwa toka mbele ya miungu yao wenyewe, walikimbilia Mesopotamia, ambako walikaa kwa muda mrefu.

9“Baada ya muda fulani, Mungu wao aliwaamuru waiache nchi ya Mesopotamia, waende kukaa katika nchi ya Kanaani. Huko wakastawi sana wakiwa na dhahabu nyingi, fedha na mifugo mingi.[#Taz Mwa 11:31–12:5]

10Njaa ilipotokea katika nchi nzima ya Kanaani, walisafiri mpaka Misri ambako walikaa wakapata chakula cha kutosha. Wakiwa huko wakawa kundi kubwa la watu - wengi hata hawakuweza kuhesabika.[#Taz Mwa 42:1-5; Kut 1:7]

11Hivyo, mfalme wa nchi ya Misri, akaanza kuwa na uhasama dhidi yao. Aliwatumia kufyatua matofali. Alishusha hadhi yao na kuwafanya watumwa.[#Taz Kut 1:8-14]

12Lakini wakamlilia Mungu wao; naye akaipiga nchi ya Misri kwa kuiletea maafa yasiyoponyeka. Basi Wamisri wakawafukuza nje ya nchi yao.[#Taz Kut 7:1-12; 29:46]

13Walipofika kwenye Bahari ya Shamu, Mungu wao akaikausha hiyo bahari mbele yao,[#Taz Kut 14:21-22]

14akawaongoza hadi kwenye mlima Sinai na Kadesh-barnea. Baada ya kuwafukuzia mbali wakazi wa jangwani;

15walifanya makao yao katika nchi ya Waamori, na kwa kutumia nguvu zao waliwaulia mbali wakazi wa Heshboni. Halafu walipovuka mto Yordani walimiliki eneo lote la milimani.

16Kisha baada ya kuwafukuza Wakanaani, Waperizi, Wayebusi, Washekemu na Wagirgashi, walikaa katika eneo hilo kwa muda mrefu.

17Wakati wote ambao hawakutenda dhambi, walistawi, maana Mungu wao ni Mungu anayechukia uovu.[#Taz Kumb 28:1-68]

18Lakini walipoiacha njia aliyowaagiza waifuate walishindwa katika vita vingi na kupelekwa mateka hadi nchi nyingine. Hekalu la Mungu wao lilibomolewa na miji yao ilikaliwa na maadui zao.

19Basi baada ya kumrudia tena Mungu wao kwanza walirudi kutoka nchi walikohamishiwa na kutawanywa. Wameushika mji wa Yerusalemu ambao kuna hekalu lao na wanaimiliki tena milima ambayo haikukaliwa na mtu.

20“Sasa bwana mkubwa, ikiwa watu hawa wamefanya kosa lolote, kama wametenda dhambi dhidi ya Mungu wao, kwanza inatupasa tuwe na uhakika kwamba ni kweli wana sababu ya kushindwa vitani, halafu tuwashambulie.

21Lakini ikiwa hawajavunja sheria yoyote, basi, na tuwaache watu hawa, tukiogopa kwamba Mungu wao atawatetea, la sivyo, sisi tutaaibika duniani kote.”

Hoja za watu

22Mara tu Akioro alipomaliza hotuba yake, watu walisimama na kuanza kupinga. Maofisa wakuu wa Holoferne, Wamoabu pamoja na watu wote kutoka pwani ya bahari ya Mediteranea walitaka Akioro auawe.

23Wakauliza, “Kwa nini tuwaogope Waisraeli, watu ambao hawana nguvu wala uwezo wa kupigana?

24Songa mbele! Endelea! Ee mkuu wetu Holoferne, jeshi lako litawameza mara moja.”

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania