Sira 31

Sira 31

Fedha huleta matatizo

1Kukosa usingizi juu ya mali humdhoofisha mtu;

kuhangaika juu yake huondoa usingizi.

2Mahangaiko ya usiku kucha hufukuza usingizi,

ni kama ugonjwa mkali, huondoa kabisa usingizi.

3Tajiri hutoa jasho na kuchuma mali nyingi,

kisha huketi chini na kuponda maisha.

4Maskini naye hutoa jasho na mali yake hupungua,

kisha huketi chini na hana chochote.

5Apendaye dhahabu hataonekana bila hatia,

na atafutaye sana fedha atapotoshwa nayo.

6Wengi wameangamia kwa sababu ya mali,

na maangamizi hayo yamewavamia ana kwa ana.

7Mali ni mtego kwa wanaovutwa nazo,

na kila mpumbavu atanaswa nazo.

8Heri mtu aliye tajiri bila kuwa na lawama,

mtu ambaye hakimbilii utajiri.

9Ni nani huyo, tumpe hongera?

Maana amefanya maajabu kati ya watu.

10Nani aliyepata kujaribiwa na mali akaonekana bila hatia?

Mtu kama huyo anayo haki kujivuna!

Nani aliyepata nafasi ya kutenda dhambi asitende?

Nani aliyepata nafasi ya kufanya maovu asifanye?

11Mtu kama huyo mali yake itadumu,

na jumuiya itautambua ukarimu wake.

Karamu

12Ukikaribishwa kwenye karamu kubwa,

usiwe na uchu mkubwa wa chakula

wala usiseme, “Kuna chakula kingi kweli!”

13Kumbuka kuwa jicho la ulafi ni kitu kibaya.

Je, kuna kitu chenye ulafi kama jicho?

Ndiyo maana jicho hutoa machozi daima.

14Usinyoshe mkono kuchukua anachotaka mwingine,

wala usimpige kumbo mwenzako kujipatia chakula.

15Tambua hali ya mwenzako unavyofikiria wewe mwenyewe,

na uwajali wengine kwa kila njia.

16Kula unachopewa kama mtu mwenye adabu,

wala usitafune harakaharaka la sivyo utachukiwa.

17Ni tabia njema kuwa wa kwanza kuacha kula,

usiwe mlafi usije ukawaudhi watu.

18Kama umeketi pamoja na watu wangu,

usiwe wa kwanza kuchukua chakula.

19Chakula kidogo ni kingi kwa mwenye adabu,

na hatahangaika akirudi nyumbani kwake.

20Mtu alaye kiasi hupata usingizi mzuri,

ataamka mapema na kujisikia mchangamfu.

Lakini mlafi atakosa usingizi,

atajisikia kichefuchefu na msokoto wa tumbo.

21Ikiwa umelazimika kula mno

ondoka ukatapike nawe utapata nafuu.

22Nisikilize mwanangu, wala usinipuuze,

na mwishowe utatambua niliyosema.

Uwe na bidii katika kazi zako zote,

nawe hutapatwa na ugonjwa wowote.

23Watu humsifu aliyemkarimu kwa chakula,

na maoni yao juu ya wema wake ni kweli.

24Mchoyo wa chakula atasemwa kijijini kote,

na maoni yao juu ya uchoyo wake ni kweli.

Pombe iliumbwa kumfurahisha mtu

25Usijioneshe kuwa hodari wa kunywa pombe,

maana pombe imewaangamiza wengi.

26Tanuri hupima ugumu wa chuma,

na pombe hupima mioyo katika shindano la wenye kiburi.

27Pombe ni kama uhai kwa mtu ukinywa kwa kiasi.

Maisha yafaa nini bila pombe?

Imeumbwa iwafurahishe watu.

28Kunywa pombe wakati wake na kwa kiasi,

kwaleta shangwe moyoni na furaha rohoni.

29Lakini kunywa pombe kupita kiasi,

kunaleta kuumwa kichwa, uchungu na fedheha.

30Ulevi huongeza hasira ya mpumbavu akajiumiza mwenyewe;

humdhoofisha na kumwongezea majeraha.

31Usimkaripie jirani yako kwenye pombe,

wala usimdharau anapofurahia karamu.

Usimwambie neno la kumwonya,

wala usimsumbue kwa kumtaka alipe deni.

Swahili Common Language DC Bible: Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki © Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya, 1995, 2001. Haki zote zimehifadhiwa.  
Published by: Bible Society of Tanzania