The chat will start when you send the first message.
1Siku zile Abia, mwana wa Yeroboamu, akaugua.[#1 Fal. 11:31.]
2Ndipo, Yeroboamu alipomwambia mkewe: Inuka, Ujigeuzegeuze, watu wasikujue, ya kuwa ndiwe mkewe Yeroboamu; kisha nenda Silo! Tazama, huko yuko mfumbuaji Ahia aliyeniambia, ya kama nitakuwa mfalme wao walio ukoo huu.
3Mkononi mwako uchukue mikate kumi na maandazi na kibuyu chenye asali, uende kwake! Yeye atakuambia yatakayokuwa ya huyu mtoto.
4Mkewe Yeroboamu akafanya hivyo, kisha akaondoka, akaenda Silo, akaingia nyumbani mwa Ahia; lakini Ahia hakuweza kuona, kwani macho yake yalikuwa yametenda kiwi kwa ajili ya uzee wake.
5Lakini Bwana alikuwa amemwambia: Tazama, mkewe Yeroboamu anakuja kukuuliza kwa ajili ya mwanawe, kwani yeye ni mgonjwa; nawe umwambie haya na haya! Naye atakapoingia atakuwa amejigeuzageuza kuwa kama mgeni.
6Ikawa, Ahia aliposikia mashindo ya miguu yake, akiingia mlangoni, akamwambia: Karibu, mke wa Yeroboamu! Mbona unajigeuzageuza kuwa kama mgeni? Nami nimetumwa kukuambia neno gumu.
7Nenda, umwambie Yeroboamu: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa Isiraeli anavyosema: Nimekutoa katikati ya watu, nikakukweza, nikakupa kuwatawala walio ukoo wangu wa Waisiraeli,[#1 Fal. 11:37; 16:2.]
8nikaunyang'anya mlango wa Dawidi ufalme, nikakupa wewe; lakini hukuwa kama mtumishi wangu Dawidi aliyeyaangalia maagizo yangu, akaendelea kunifuata kwa moyo wake wote mzima, ayafanye hayo tu yanyokayo machoni pangu.
9Lakini umefanya mabaya kuliko wote waliokuwa mbele yako, kwani umejiendea, ukajitengenezea miungu mingine na vinyago, unikasirishe, ukanitupa nyuma yako.
10Lakini mtaniona, nikiuletea mlango wa Yeroboamu mabaya, niwatoweshe wa kiume walio wa Yeroboamu, kama watakuwa wamefungwa au kama watakuwa wamefunguliwa kwao Waisiraeli, nitawazoa walio wa mlango wa Yeroboamu, kama watu wanavyozoa mavi, hata wamalizike kabisa.[#1 Fal. 15:29; 21:21.]
11Wao wa Yeroboamu watakaokufa mjini mbwa watawala; nao watakaokufa shambani madege wa angani watawala, kwani Bwana amevisema.[#1 Fal. 16:4; 21:24.]
12Nawe inuka, uende nyumbani kwako! Hapo, miguu yako itakapoingia mjini, papo hapo mtoto atakufa.
13Waisiraeli wote watamwombolezea, kisha watamzika, kwani kwao wa Yeroboamu huyu peke yake ndiye atakayeingia kaburini, kwani katika mlango wa Yeroboamu ni kwake tu kulikoonekana yaliyokuwa mema machoni pa Bwana.
14Yeye Bwana atajiinulia mfalme wa Waisiraeli atakayeutowesha huu mlango wa Yeroboamu siku hiyo, nayo ya sasa siyo yayo hayo?[#1 Fal. 15:29.]
15Ndipo, Bwana atakapowapiga Waisiraeli, kama matete yanavyotikiswa majini; atawang'oa Waisiraeli katika nchi hii njema, aliyowapa baba zao, awatawanye ng'ambo ya lile jito kubwa, kwa kuwa wamejitengenezea miti ya Ashera inayomkasirisha Bwana.[#2 Fal. 17:23.]
16Atawatoa Waisiraeli kwa ajili ya makosa, Yeroboamu aliyoyakosa na kuwakosesha Waisiraeli nao.[#1 Fal. 12:30; 13:34.]
17Kisha mkewe Yeroboamu akaondoka, akaenda zake kufika Tirsa; alipoingia penye kizingiti cha nyumba, ndipo, yule kijana alipokufa.
18Wakamzika, nao Waisiraeli wote wakamwombolezea, kama Bwana alivyosema kinywani mwa mtumishi wake mfumbuaji Ahia.
19Mambo mengine ya Yeroboamu, jinsi alivyopiga vita, tena alivyotawala, tunayaona, yameandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Waisiraeli.
20Siku, Yeroboamu alizokuwa mfalme, ni miaka 22; kisha akaja kulala na baba zake, naye mwanawe Nadabu akawa mfalme mahali pake.[#1 Fal. 15:25.]
21Rehabeamu, mwana wa Salomo, akapata kuwa mfalme wa Wayuda; yeye Rehabeamu alikuwa mwenye miaka 41 alipoupata ufalme, akawa mfalme miaka 17 mle Yerusalemu katika ule mji, Bwana aliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, alikalishe Jina lake humo. Jina la mama yake ni Nama aliyekuwa Mwamoni.[#1 Fal. 12:17.]
22Wayuda wakayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wakamchokoza kwa makosa yao, waliyoyakosa, maana yalikuwa mabaya kuliko yote, baba zao waliyoyafanya.
23Nao wakajijengea vijumba vya kutambikia vilimani, wakajitengenezea nguzo za kutambikia na miti ya Ashera juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mengi.[#2 Fal. 16:4.]
24Hata wagoni wa patakatifu pao walikuwako katika nchi, wakayafanya matapisho yote ya wamizimu, Bwana aliowafukuza mbele yao Waisiraeli.[#5 Mose 23:17.]
25Katika mwaka wa tano wa mfalme Rehabeamu ndipo, Sisaki, mfalme wa Misri, alipopanda kuujia Yerusalemu.[#1 Fal. 11:40.]
26Akavichukua vilimbiko vya Nyumbani mwa Bwana navyo vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme, vyote pia akavichukua, nazo ngao za dhahabu, Salomo alizozitengeneza, akazichukua.[#1 Fal. 10:16.]
27Mahali pao mfalme Rehabeamu akatengeneza ngao za shaba, akazitia mikononi mwa wakuu wa wapiga mbio waliongoja pa kuingia nyumbani mwa mfalme, waziangalie.
28Kila mara, mfalme alipoingia Nyumbani mwa Bwana, wapiga mbio wakazichukua, kisha wakazirudisha chumbani mwao wapiga mbio.
29Mambo mengine ya Rehabeamu nayo yote, aliyoyafanya, hayakuandikwa katika kitabu cha mambo ya siku za wafalme wa Wayuda?
30Navyo vita vya kupigana kwao Rehabeamu na Yeroboamu vilikuwako siku zote.[#1 Fal. 15:6.]
31Rehabeamu akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi, nalo jina la mama yake ni Nama aliyekuwa Mwamoni. Naye mwanawe Abiamu akawa mfalme mahali pake.[#1 Fal. 14:21.]