Mpiga mbiu 10

Mpiga mbiu 10

Werevu wa kweli na ujinga huwa kwa wakuu na kwa wadogo.

1Mainzi waliokufa huyaozesha kwa kuyachafua mafuta ya mtengeneza manukato, ujinga hufanya makuu kuliko werevu wa kweli na utukufu.

2Moyo wa mwerevu wa kweli huelekea kuumeni, lakini moyo wa mjinga huelekea kushotoni.

3Napo njiani po pote, mjinga anapokwenda, hupotelewa na akili, hivyo hujitokeza kwao wote kuwa mjinga.

4Roho ya mtawalaji ikikuinukia, usiondoke mahali pako, kwani upole hutuliza makosa makubwa.[#Sh. 37:1; Fano. 24:19.]

5Yako mabaya, niliyoyaona chini ya jua, ni kama kosa litokalo kwake mwenye ukuu:

6ni mjinga akitukuzwa sana, nao wenye mali wakikaa na kunyenyekezwa.[#Fano. 30:21-22.]

7Nikaona nao watumishi wanaopanda farasi, wakuu wakienda na kukanyaga nchi kama watumishi.

8Achimbaye mwina hutumbukia humo, naye abomoaye boma huumwa na nyoka.[#Fano. 26:27.]

9Avunjaye mawe huumizwa nayo, naye achanjaye kuni hujiponza papo hapo.

10Chuma kikiwa kimedugika, naye mwenyewe hakinoi, kipate makali, hana budi kutumia nguvu zaidi; hapo napo werevu wa kweli hufaa kwa kufanikiwa.

11Nyoka akiuma mtu, akiwa hajatabanwa, bado, basi, mwenye kutabana hanacho, anachokipata.[#Sh. 58:5-6.]

12Maneno ya kinywa chake mwerevu wa kweli hupendeza, lakini midomo ya mjinga hummeza.

13Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni ujinga, nao mwisho ni kusema upuzi mbaya.

14Yeye mjinga husema mengi; lakini hakuna mtu ayajuaye yatakayokuwa, tena yuko nani awezaye kumweleza yatakayokuwa nyuma yake?[#Mbiu. 5:3; 8:7.]

15Masumbuko, anayoyasumbuka mjinga, humchokesha, kwa kuwa hajui hata njia ya kwenda mjini.

16Utaona mabaya, wewe nchi, mfalme wako akiwa kijana, nao wakuu wako wakila na mapema.[#Yes. 3:4.]

17Utaona mema, wewe nchi, mfalme wako akiwa mwana wa watu wenye macheo, nao wakuu wako wakila hapo panapopasa, wapate nguvu za kiume, wasile kwa kujilewesha.

18Kwa ajili yao wajengao kwa uvivu kipaa huinama, kwa ulegevu wa mikono nyumba huvuja.[#Fano. 19:15.]

19Watu hufanya karamu, wapate kucheka, nayo mvinyo huwafurahisha walioko huku nchini, nazo fedha hupata yote.[#Amu. 9:13; Sh. 104:15.]

20Mfalme usimtukane hata kwa mawazo yako! Wala chumbani mwako, unamolala, usimtukane mwenye mali! Kwani ndege wa angani watayapeleka, uliyoyasema, naye mwenye mabawa atayatangaza hayo maneno.[#2 Mose 22:28.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania