Mpiga mbiu 2

Mpiga mbiu 2

Furaha zote huku nchini ni za bure.

1Nilisema moyoni mwangu: Haya! Niyajaribu yenye furaha, nijionee mema! Nikaona, hayo nayo ni ya bure.

2Macheko nikayaambia: Ni kuwa na wazimu, nayo furaha nikaiambia: Hii inafaaje?

3Niliwaza moyoni mwangu kuufurahisha mwili wangu kwa mvinyo, lakini akili zikae zikiuongoza mwili; nikataka kuufuata huo ujinga, mpaka niyaone yawafaliayo wana wa Adamu kuyafanya chini ya mbingu siku zao zote za kuwapo.[#Fano. 31:4.]

4Matendo yangu, niliyoyafanya, yakawa makubwa: nilijijengea nyumba, nikajipandia mizabibu.

5Nikajitengenezea mashamba na vimwitu, nikapanda humo miti ya matunda ya kila namna.

6Nikajitengenezea nayo maziwa ya maji ya kunyweshea mwitu, uichipuze miti.

7Nikajipatia watumishi na vijakazi, nikawa nao watumwa waliozaliwa nyumbani mwangu, nikawa na makundi ya ng'ombe na ya kondoo kuliko wote waliokuwako mbele yangu Yerusalemu.

8Nikajikusanyia nazo fedha na dhahabu zilizokuwa mali za wafalme wengine na za nchi nyingine, nikajipatia waimbaji waume na wake, tena wana wa Adamu wanaowatunukia sana, mabibi wengi sana.

9Hivyo nikawa mkuu zaidi kuwashinda wote pia waliokuwako mbele yangu Yerusalemu, nao werevu wangu wa kweli ukakaa kwangu.[#1 Fal. 10:23.]

10Yote, macho yangu yaliyoyatamani, hakuna nilichoyanyima; wala moyo wangu sikuukataza furaha yo yote. Kwani moyo wangu uliyafurahia yote, niliyoyasumbukia, tena furaha hii ilikuwa pato langu, nililojipatia kwa masumbuko yangu yote.

11Lakini nilipogeuka kuzitazama kazi zote, mikono yangu ilizozifanya, tena nilipoyakumbuka hayo masumbuko, niliyoyasumbuka kwa kuyafanya yale, ndipo, nilipoona, yote ni ya bure, ni kuukimbilia upepo, hakuna pato, mtu analojipatia chini ya jua.[#Mbiu. 1:14.]

12Kisha mimi nikageuka kuupambanua werevu wa kweli na upumbavu na ujinga; kwani mtu atakayemfuata mfalme atafanya nini? Ni yale yale, watu waliyoyafanya tangu kale.[#Mbiu. 1:17.]

13Mimi nikatazama, kama liko, ambalo werevu wa kweli unaupita ujinga, nikaona kuwa sawa, kama mwanga unavyoipita giza.

14Mwerevu wa kweli anayo macho yake kichwani mwake, naye mjinga huenda gizani; lakini papo hapo nikatambua nayo haya, ya kuwa jambo la mwisho linalowapata wao wote ni lilo hilo moja.[#Fano. 17:24.]

15Nikasema moyoni mwangu: Kama jambo la mwisho linalompata mjinga ni lilelile litakalonipata mimi nami, werevu wangu wa kweli uliozidi sana ni wa nini? Nikasema moyoni mwangu: Huu nao ni wa bure.

16Kwani wala mwerevu wa kweli wala mjinga atakumbukwa kale na kale; kwani katika siku zijazo wote pia watakuwa wamesahauliwa. Kumbe mwerevu wa kweli hufa sawasawa kama mjinga![#Sh. 49:11.]

17Nikachukizwa na kuwapo, kwani kazi zinazofanywa chini ya jua zikawa mbaya machoni pangu, kwani zote ni za bure, ni za kuukimbilia upepo.

18Ndipo, mimi nilipochukizwa na masumbuko yangu yote niliyoyasumbuka chini ya jua, kwani niliyoyasumbukia nitamwachia mtu atakayekuwapo nyuma yangu.[#Mbiu. 2:21,26; Sh. 39:7.]

19Tena yuko nani anayejua, kama atakuwa mwerevu wa kweli au mjinga? Lakini atayatawala yote, niliyojipatia chini ya jua kwa usumbufu wangu na kwa werevu wangu wa kweli. Kwa hiyo nayo ni ya bure.

20Ndipo, nilipotangatanga na kuzikata tamaa zote za moyo wangu kwa ajili ya masumbuko, niliyoyasumbuka chini ya jua.

21Kwani huwa hivyo: mtu aliyejisumbua kwa werevu wa kweli na kwa ujuzi na kwa kufanikiwa humpa fungu lake mtu asiyelisumbukia. Hayo nayo ni ya bure na mabaya sana.

22Kwani kiko kitu gani, mtu anachokipata kwa masumbuko yake yote na kwa bidii za moyo wake, ulizozifanya na kusumbuka chini ya jua?

23Kwani siku zake zote ni za maumivu, nao utumishi wake ni wenye masikitiko, moyo wake usiweze kutulia nao usiku; hayo nayo ni ya bure.

24Basi, hakuna mema ya mtu kuliko kula na kunywa na kuipatia roho yake mema katika masumbuko yake. Lakini haya nayo nikayaona, ya kuwa hutoka mkononi mwa Mungu tu.[#Mbiu. 3:12,22; 5:18; 8:15; 9:7.]

25Kwani yuko nani awezaye kula na kujifurahisha, huyu akiwa hayuko?

26Kwani mtu aliye mwema machoni pake humpa werevu wa kweli na ujuzi na furaha; lakini aliye mkosaji humpa utumishi wa kukusanya na kulimbika, ampe yule aliye mwema machoni pake Mungu. Hayo nayo ni ya bure na kuukimbilia upepo.[#Fano. 13:22; 28:8.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania