Ezera 6

Ezera 6

Nyumba ya Mungu inamalizwa, kisha inaeuliwa.

1Ndipo, mfalme Dario alipotoa amri, wakachunguza nyumbani mwenye vitabu, mlimowekwa navyo vilimbiko vya huko Babeli.

2Kisha kikaoneka kizingo cha karatasi katika mji wa Ahimeta katika nchi ya Media; ndimo, nalo jumba la mfalme lilimokuwa. Ile karatasi ilikuwa imeandikwa: Ukumbusho.

3Kwamba: Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Kiro huyu mfalme Kiro akatoa amri, Nyumba ya Mungu huko Yerusalemu na ijengwe kuwa mahali, watakapotoa ng'ombe za tambiko, misingi yake itengenezwe kuwa na nguvu; urefu wake uwe mikono sitini, nao upana wake uwe mikono sitini.[#Ezr. 1:1.]

4Waweke masafu matatu ya mawe makubwa ya kuchonga, tena safu moja la mbao mpya; nazo fedha za kulipa wapewe, zitoke nyumbani mwa mfalme.

5Navyo vyombo vya Nyumba ya Mungu vya dhahabu na vya fedha, Nebukadinesari alivyovitoa Nyumbani mle Yerusalemu na kuvipeleka Babeli, sharti virudishwe, vije Nyumbani mwa Yerusalemu kila kimoja mahali pake na kuwekwa mle Nyumbani mwa Mungu.

6Sasa wewe Tatinai, mtawala nchi zilizoko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, na Setari-Bozinai pamoja na wenzako Waafarsaki walioko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, jitengeni, msifike huko!

7Waacheni, kazi za Nyumba hii ya Mungu ziendelee, mtawala nchi wa Wayuda na wazee wa Wayuda waijenge Nyumba hiyo ya Mungu hapo, ilipokuwa!

8Mimi natoa amri, ya kwamba msaidiane na hao wazee katika kuijenga Nyumba hiyo ya Mungu, mkifanya bidii, mpate kutoa mali za mfalme zitokazo katika kodi za nchi zilizoko ng'ambo ya huko ya jito kubwa, watu hao wapewe kila mara fedha za kuzilipa hizo hazi, wasizuiliwe.

9Nayo mengine wanayopaswa nayo, kama madume ya ndama na madume ya kondoo na wana kondoo wa kuwa ng'ombe za tambiko za Mungu wa mbingu, tena ngano na chumvi na mvinyo na mafuta, kama watambikaji walioko Yerusalemu wanavyovitaka, sharti wapewe siku kwa siku, visikoseke,

10wapate kumtolea mungu wa Mbingu minuko mizuri na kuwaombea wafalme na wana wao, wawe wenye uzima.

11Tena ninatoa amri kwamba: Kila mtu atakayeligeuza neno hili nyumbani mwake itolewe nguzo, isimikwe, kisha mwenyewe atundikwe humo, nayo nyumba yake igeuzwe kuwa kifusi kwa ajili hiyo.

12Naye Mungu atakayelikalisha Jina lake mle na awabwage chini wafalme wote na watu wote watakaokunjua mikono yao, waligeuze neno hili, waiharibu Nyumba hiyo ya Mungu iliyomo Yerusalemu. Mimi Dario nimeitoa amri hii, sharti ifanyizwe pasipo kuikosea.

13Kwa hiyo Tatinai, mtawala nchi zilizoko ng'ambo ya huku ya jito kubwa, na Setari-Bozinai na wenzao wakafanya sawasawa kabisa, kama mfalme Dario alivyowaagiza katika hiyo barua.

14Nao wazee wa Wayuda wakaendelea kujenga, wakafanikiwa, kama wafumbuaji Hagai na Zakaria, mwana wa Ido, walivyowaambia kwa ufumbuaji wao: wakajenga, hata wakamaliza kwa amri yake Mungu wa Isiraeli na kwa amri za Kiro na za Dario na za Artasasta, wafalme wa Wapersia.

15Nyumba hii ikamalizika siku ya tatu ya mwezi wa Adari, nao ule mwaka ulikuwa wa sita wa ufalme wa mfalme Dario.[#Ezr. 4:24.]

16Ndipo, wana wa Isiraeli, watambikaji na Walawi nao wale wengine waliotoka kwenye kutekwa walipoieua Nyumba hii ya Mungu kwa furaha.[#4 Mose 7:10; 1 Fal. 8:62-66.]

17Hapo walipoieua Nyumba hii ya Mungu wakatoa ng'ombe 100 na madume ya kondoo 200 na wana kondoo 400 kuwa ng'ombe za tambiko, tena madume 12 ya mbuzi kwa hesabu ya mashina ya Isiraeli kuwa ng'ombe za tambiko za weuo wa ukoo mzima wa Isiraeli.[#Ezr. 8:35.]

18Kisha wakaweka watambikaji kwa vyama vyao nao Walawi kwa kura zao, walizopigiwa, wamtumikie Mungu mle Yerusalemu, kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mose.[#4 Mose 3:6; 8:24.]

Sikukuu ya Pasaka.

19Kisha wao waliotoka kwenye kutekwa wakafanya sikukuu ya Pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi wa kwanza.[#2 Mose 12:6.]

20Kwani watambikaji na Walawi walijitakasa pamoja, wakatakata wote pia, wakawachinjia kondoo wa Pasaka wote waliotoka kwenye kutekwa nao ndugu zao watambikaji nao wao wenyewe.

21Wana wa Isiraeli waliorudi kwenye kutekwa wakaila pamoja nao waliotaka kumfuata Bwana Mungu wa Isiraeli, waliojitenga, wasijichafue kwa wamizimu wenzao waliokaa kwao katika nchi hii.

22Wakaifanya hiyo sikukuu ya Mikate isiyochachwa siku saba na kufurahi, kwani Bwana aliwafurahisha kwa kuugeuza moyo wa mfalme wa Asuri, uwaelekee, aishupaze mikono yao katika kazi ya Nyumba ya Mungu aliye Mungu wa Isiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania