Waamuzi 3

Waamuzi 3

Mataifa yaliyosalia katika nchi ya Kaanani.

1Haya ndiyo mataifa, Bwana aliyoyaacha, wakae, awatumie kuwajaribu Waisiraeli wote wasioyajua mapigano yote ya Kanaani.[#Amu. 2:22.]

2Huko ni kwamba tu: vizazi vingine vya wana wa Isiraeli wayajue, wapate kujifundisha mapigano, ni wale tu wasioyajua mapigano ya kale.

3Nayo mataifa ni haya: watawalaji watano wa Wafilisti na Wakanaani wote na Wasidoni na Wahiwi waliokaa milimani kwa Libanoni kutoka kwenye mlima wa Baali-Hermoni mpaka kufika Hamati.[#Yos. 13:3.]

4Hao ndio, aliowataka wa kuwajaribu Waisiraeli, ajue, kama watayasikia maagizo ya Bwana, aliyowaagiza baba zao kinywani mwa Mose.

5Ndivyo, wana wa Isiraeli walivyokaa katikati kwao Wakanaani na kwa Wahiti na kwa Waamori na kwa Waperizi na kwa Wahiwi na kwa Wayebusi.

6Wakawachukua wana wao wa kike, wawe wake zao, nao wana wao wa kike wakawapa wana wao wa kiume, nayo miungu yao wakaitumikia.[#5 Mose 7:3.]

Mwamuzi wa kwanza Otinieli.

7Wana wa Isiraeli walipoyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, wakimsahau Bwana Mungu wao, watumikie vinyago vya Baali na vya Ashera,

8makali ya Bwana yakawawakia Waisiraeli, akawauza na kuwatia mkononi mwa Kusani-Risataimu, mfalme wa Mesopotamia; nao wana wa Isiraeli wakamtumikia Kusani-Risataimu miaka 8.

9Wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia wana wa Isiraeli mwokozi, awaokoe, ndiye Otinieli, mwana wa Kenazi, mdogo wake Kalebu.[#Amu. 1:13.]

10Roho ya Bwana ilipomjia, akawa mwamuzi wa Waisiraeli, akatoka kwenda vitani, naye Bwana akamtia Kusani-Risataimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake, kwa kuwa mkono wake yeye ulikuwa wenye nguvu kuliko ule wa Kusani-Risataimu.[#Amu. 6:34.]

11Ndipo, nchi ilipopata kutulia miaka 40, kisha Otinieli, mwana wa Kenazi, akafa.

Mwamuzi Ehudu.

12Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Bwana akamtia Egloni, mfalme wa Moabu, nguvu, awashinde Waisiraeli, kwa kuwa waliyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana.

13Ndipo, alipokusanya kwake wana wa Amoni na Waamaleki, kisha akaenda, akawapiga Waisiraeli, nao Mji wa Mitende wakauchukua.[#Amu. 1:16.]

14Kisha Waisiraeli wakamtumikia Egloni, mfalme wa Moabu, miaka 18.

15Wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia mwokozi, ndiye Ehudu, mwana wa Gera wa Benyamini, ni mtu mwenye shoto. Huyu wana wa Isiraeli wakamtuma kumpelekea Egloni, mflame wa Moabu, mahongo.

16Ehudu akajipatia upanga wenye ukali pande zote mbili, nao urefu wake kama mkono; akaufunga chini ya nguo yake penye paja lake la kuume.

17Akampelekea Egloni, mfalme wa Moabu, hayo mahongo, naye Egloni alikuwa mtu mnene sana.

18Alipokwisha kumpelekea hayo mahongo, akawapa wale watu waliochukua mahongo ruhusa kwenda zao.

19Lakini mwenyewe akarudia Gilgali, hapo palipokuwa na vinyago, akasema: Nina neno la njama na wewe mfalme; naye akasema: Nyamaza kwanza! Wote waliosimama kwake walipokwisha kutoka,

20Ehudu akaingia mwake; naye alikuwa amekaa katika chumba cha juu chenye baridi yeye peke yake tu. Ehudu aliposema: Ninalo neno la Mungu la kukuambia, akainuka katika kiti chake cha kifalme.

21Ndipo, Ehudu alipoupeleka mkono wake wa kushoto, akauchomoa upanga penye paja lake la kuume, akamchoma tumboni;

22hata kipini kikaingia ndani pamoja na chuma cha upanga, nayo mafuta yakapafungia palipoingia upanga, kwani hakuutoa upanga tumboni, nao ulitokea nyuma.

23Kisha Ehudu akatoka, akaja barazani, akaifunga milango ya kile chumba cha juu nyuma yake kwa komeo.

24Alipokwisha kutoka, watumishi wake Egloni wakaja; lakini walipoona, ya kuwa milango ya chumba cha juu imefungwa kwa makomeo, wakasema; Labda amejifunika miguu yake katika chumba cha baridi.

25Wakangoja kwa kuona soni, lakini walipoona ya kuwa hakuna anayeifungua milango ya chumba, wakachukua ufunguo, wakaifungua, mara wakamwona bwana wao, akilala chini, maana amekufa.

26Naye Ehudu alikuwa ameponyoka, wale walipokawilia, naye akapapita penye vinyago, akapona kweli alipofika Seira.

27Alipoingia humo akapiga baragumu milimani kwa Efuraimu; ndipo, wana wa Isiraeli waliposhuka pamoja naye kutoka milimani, naye akawaongoza.

28Akawaambia: Nifuateni upesi! Kwani Bwana amewatia adui zenu, hawa Wamoabu, mikononi mwenu. Ndipo, waliposhuka na kumfuata, wakavivuka vivuko vya Yordani penye njia za kwenda Moabu, kisha hawakumpa mtu ruhusa kuvuka.

29Wakati huo wakaua Wamoabu kama watu 10000, wote waliokuwa wanene nao wenye nguvu wote, hakuwako aliyepona.

30Siku hiyo Wamoabu wakanyenyekezwa kuwa chini ya mikono ya Waisiraeli; ndipo, nchi ilipopata kutulia miaka 80.

Mwamuzi Samugari.

31Aliyemfuata ni Samugari, mwana wa Anati; akaua Wafilisti watu 600 kwa fimbo tu la kuchungia ng'ombe; hivyo yeye naye aliwaokoa Waisiraeli.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania