The chat will start when you send the first message.
1Wana wa Isiraeli walipoendelea kuyafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana, Ehudu alipokwisha kufa,
2Bwana akawauza na kuwatia mikononi mwa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala Hasori; naye mkuu wa vikosi vyake alikuwa Sisera, naye alikaa Haroseti wa Wamizimu.
3Ndipo, wana wa Isiraeli walipomlilia Bwana, kwani alikuwa na magari ya chuma 900, naye aliwatesa wana wa Isiraeli kwa nguvu miaka 20.
4Wakati huo kulikuwako mfumbuaji wa kike, jina lake Debora, mkewe Lapidoti, naye alikuwa mwamuzi wa Waisiraeli.
5Huyu Debora alikaa chini ya mtende wake katikati ya Rama na Beteli milimani kwa Efuraimu, nao wana wa Isiraeli wakapanda kuja kwake kuamuliwa.
6Naye akatuma kumwita Baraka, mwana wa Abinoamu wa Kedesi katika nchi ya Nafutali, akamwambia: Bwana Mungu wa Isiraeli hakukuagiza: Nenda kushika njia ya kwenda mlimani kwa Tabori, uchukue kwao wana wa Nafutali nako kwao wana wa Zebuluni watu 10000 wa kwenda na wewe?
7Nawe utakapofika mtoni kwa Kisoni, mimi nitamtuma Sisera, mkuu wa vikosi vya Yabini, afike kwako na magari yake na mtutumo wa watu wake, nimtie mkononi mwako.
8Baraka akamwambia: Ukienda pamoja nami, basi, nitakwenda. lakini usipokwenda pamoja nami, sitakwenda.
9Akamwambia: Nitakwenda pamoja na wewe; lakini ujue: matukuzo ya njia hii, unayokwenda, hayatakuwa yako, kwani Bwana atamtia Sisera mkononi mwa mwanamke. Kisha Debora akaondoka, akaenda Kedesi pamoja na Baraka.
10Baraka akawaita watu wa Zebuluni na wa Nafutali kuja Kedesi. Alipopata watu 10000 kwenda naye kwa miguu yao, Debora akaenda naye kupanda huko.
11Lakini Mkeni Heberi alikuwa amejitenga na Wakeni wenzake, wale wana wa Hobabu, shemeji yake Mose, akalipiga hema lake kwenye mvule wa Sananimu karibu ya Kedesi.[#Amu. 1:16; 4 Mose 10:29.]
12Watu walipompasha Sisera habari, ya kuwa Baraka, mwana wa Abinoamu, ameupanda mlima wa Tabori,
13Sisera akaagiza, magari yake yote ya chuma 900 yakusanywe, nao watu wake wote watoke Haroseti wa Wamizimu, waje mtoni kwa Kisoni.
14Ndipo, Debora alipomwambia Baraka: Inuka! Kwani hii ndiyo siku, Bwana atakayomtia Sisera mkononi mwako! Je? Bwana hakutoka mwenyewe kukuongoza? Kisha Baraka akashuka mlimani kwa Tabori, nao watu wake 10000 wakamfuata.
15Bwana akamstusha Sisera, akiyavuruga magari yote na majeshi yote kwa ukali wa panga machoni pake Baraka; ndipo, Sisera aliposhuka garini mwake, akimbie kwa miguu.
16Naye Baraka akayafuata mbiombio magari na majeshi mpaka Haroseti wa Wamizimu; ndiko, hayo majeshi yote ya Sisera walikopigwa kwa ukali wa panga, hakusalia hata mmoja.
17Naye Sisera alipokimbia kwa miguu yake akalikimbilia hema la Yaeli, mkewe Heberi, yule Mkeni, kwani Yabini, mfalme wa Hasori, na mlango wa Mkeni Heberi walikuwa wanapatana.
18Yaeli akatoka kumwendea Sisera njiani, akamwambia: Njoo, bwana wangu! Jiingilie mwangu, usiogope! Ndipo, alipoingia hemani mwake, naye akamfunika kwa blanketi.
19Kisha akamwambia: Nipe maji kidogo, ninywe! Kwani nina kiu. Akafungua kiriba cha maziwa, akamnywesha, kisha akamfunika tena.
20Akamwambia: Simama langoni mwa hema! Kama mtu anakuja kukuuliza kwamba: Yumo mtu? mwambie: Hapana!
21Kisha Yaeli, mkewe Heberi, akachukua uwambo mmoja wa hema, akatwaa nayo nyundo mkononi mwake, akamjia polepole, akaupigilia ule uwambo pajini kichwani, mpaka uingie mchangani, maana alikuwa amelala usingizi kabisa; ndipo, alipozimia, akafa.
22Mara akatokea Baraka aliyemfuata Sisera mbiombio, naye Yaeli akatoka kumwendea njiani, akamwambia: Njoo, nikuonyeshe yule mtu, unayemtafuta! Alipoingia mwake akamwona Sisera, akilala chini hivyo, alivyokufa, nao uwambo umo pajini.
23Siku hiyo ndipo, Mungu alipomnyenyekeza Yabini, mfalme wa Kanaani, machoni pao wana wa Isiraeli; nayo mikono yao wana wa Isiraeli ikazidi kumlemea Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka wakimwangamiza kabisa huyo Yabini, mfalme wa Kanaani.