The chat will start when you send the first message.
1Mkutano wote wa wana wa Isiraeli ukakusanyika huko Silo, wakapanga huko lile Hema la Mkutano, kwani nchi hii ilikuwa imekwisha kushindwa nao.[#Amu. 21:19; 1 Sam. 1:3; 4:4.]
2Lakini kwao wana wa Isiraeli walikuwako mashina saba wasiopata bado mafungu yao ya nchi.
3Ndipo, Yosua alipowaambia wana wa Isiraeli: Mpaka lini ninyi mtailegeza mikono yenu, msiende kuichukua nchi hii, Bwana Mungu wa baba zenu aliyowapa?
4Haya! Jichagulieni kila shina watu watatu, niwatume, waondoke kwenda katika nchi hiyo, waiandike hiyo itakayokuwa fungu lao! Kisha watakaporudi kwangu,
5waigawanye, itoke mafungu saba, Wayuda wakiushika mpaka wao upande wa kusini nao wa mlango wa Yosefu wakiushika wao mpaka upande wa kaskazini.
6Ninyi mtakapokwisha kuiandika nchi, itoke mafungu saba, mniletee hapa huo mwandiko! Ndipo, nitakapowapigia kura hapa machoni pa Bwana Mungu wetu.
7Kwani Walawi hawatapata fungu katikati yenu, kwani utambikaji wa Bwana ndio fungu lao; nao Wagadi na Warubeni na nusu ya Wamanase wamekwisha kuyachukua mafungu yao ng'ambo ya huko ya Yordani upande wa maawioni kwa jua, aliyowapa Mose, mtumishi wa Bwana.[#Yos. 13:14-33.]
8Ndipo, watu wale walipoondoka kwenda zao, nao waliokwenda kuiandika nchi Yosua akawaagiza kwamba: Nendeni kuzunguka katika nchi hiyo na kuiandika! Kisha rudini kwangu! Ndipo, nitakapowapigia kura machoni pa Bwana hapa Silo.
9Wale watu wakaenda, wakapita po pote katika hizo nchi, wakaziandika katika kitabu, mji kwa mji, zipate kutokea kuwa mafungu saba, kisha wakarudi makambini kwa Yosua huko Silo.
10Ndipo, Yosua alipowapigia kura huko Silo machoni pa Bwana; ndivyo, Yosua alivyowagawanyia wale wana wa Isiraeli hizo nchi, wayapate mafungu yao.
11Ikatokea kura ya shina la wana wa Benyamini ya kuzigawanyia koo zao, nayo nchi, kura iliyowapatia, ilikuwa katikati ya wana wa Yuda na wana wa Yosefu.
12Mpaka wao wa upande wa kaskazini ulitoka mtoni kwa Yordani, kisha mpaka ulipanda kandokando ya Yeriko upande wake wa kaskazini, tena uliendelea kupanda milimani upande wa baharini, utokee katika nyika ya Beti-Aweni.[#Yos. 7:2.]
13Toka huko mpaka uliendelea kufika Luzi, kando ya Luzi kuelekea kusini, nao Luzi ndio Beteli; kisha mpaka ulishukia Ataroti-Adari katika ule mlima ulioko upande wa kusini wa Beti-Horoni wa chini.
14Kisha mpaka uliendelea na kugeuka upande wake wa baharini, uelekee kusini toka mlima huo unaoelekea Beti-Horoni upande wa kusini, utokee Kiriati-Baali, ndio Kiriati-Yearimu ulio mji wa wana wa Yuda. Huu ndio upande wake wa kuelekea baharini.[#Yos. 15:6-9.]
15Nao upande wake wa kuelekea kusini ulianza pembeni kwa Kiriati-Yearimu; mpaka ulipotoka huko uliendelea upande wa baharini kufika kwenye chemchemi ya maji ya Nefutoa.
16Toka huko mpaka ulitelemka kufika pembeni kwa mlima ule unaoelekea bondeni kwa mwana wa Hinomu ulioko upande wa kaskazini wa Bonde la Majitu, ulishuka Bondeni kwa Hinomu kando kwao Wayebusi upande wao wa kusini, tena uliendelea kushuka Eni-Rogeli.
17Toka huko mpaka uliendelea na kugeukia kaskazini na kutoka Eni-Semesi, ulitokea Geliloti unaoelekea hapo pa kukwelea Adumimu, kisha ulishuka kwenye mwamba wa Bohani, mwana wa Rubeni.
18Toka huko mpaka uliendelea na kupita upande wa kaskazini kando ya kilima kinachoelekea Araba, kisha ulitelemkia hapo Araba;
19kisha mpaka uliendelea na kupita kando ya Beti-Hogla upande wa kaskazini, upate kutokea pembeni kwa Bahari ya Chumvi upande wake wa kaskazini kwenye mwisho wa kusini wa Yordani. Huu ndio mpaka wa kusini.
20Lakini Yordani ulikuwa mpaka wake wa upande wa maawioni kwa jua. Hili lilikuwa fungu lao wana wa Benyamini la kuzigawanyia koo zao, mipaka yake ilivyolizunguka.
21Miji ya shina la wana wa Benyamini ya kuzigawanyia koo zao ilikuwa: Yeriko na Beti-Hogla na Emeki-Kesisi,
22na Beti-Araba na Semaraimu na Beteli,
23na Awimu na Para na Ofura,
24na Kefari-Amoni na Ofuni na Geba; ndio miji 12 pamoja na mitaa yao.
25Gibeoni na Rama na Beroti,
26na Misipe na Kefira na Mosa,
27na Rekemu na Iripeli na Tarala,
28na Sela, na Elefu na Yebusi, ndio Yerusalemu, Gibeati, Kiriati, ndio miji 14 pamoja na mitaa yao. Hili lilikuwa fungu lao wana wa Benyamini la kuzigawanyia koo zao.[#Yos. 15:63; Amu. 1:21.]