The chat will start when you send the first message.
1Baada ya siku sita Yesu akamchukua Petero na Yakobo na Yohana nduguye, akapanda pamoja nao peke yao juu ya mlima mrefu.
2Huko akageuzwa sura yake machoni pao. Uso wake ukamulika kama jua, nazo nguo zake zikamerimeta kama mwanga.[#2 Petr. 1:16-18.]
3Walipotazama, wametokewa na Mose na Elia, wanaongea na Yesu.
4Petero akasema akimwambia Yesu: Bwana, hapa ni pazuri kuwapo sisi. Ukitaka, nitajenga hapa vibanda vitatu; kimoja chako, na kimoja cha Mose, na kimoja cha Elia.
5Angali akisema, mara wingu jeupe likawatia kivuli, sauti ikatoka winguni, ikisema: Huyu ndiye mwanangu mpendwa, ambaye nimependezwa naye. Msikilizeni yeye![#Mat. 3:17; 2 Petr. 1:16-18.]
6Wanafunzi walipoyasikia wakaanguka kifudifudi, wakaingiwa na woga sana.
7Yesu akawaendea, akasema akiwagusa: Inukeni, msiogope!
8Walipoyainua macho yao, hakuna waliyemwona, asipokuwa Yesu peke yake.
9Walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaagiza akisema: Msimwambie mtu ye yote mliyoyaona, mpaka Mwana wa mtu atakapofufuliwa katika wafu!*[#Mat. 16:20.]
10Nao wanafunzi wakamwuliza wakisema: Basi, waandishi husemaje: Sharti kwanza Elia aje?[#Mat. 11:14; Mal. 4:5.]
11Naye akajibu akisema: Kweli Elia anakuja, vyote avigeuze kuwa vipya.[#Luk. 1:17.]
12Lakini nawaambiani: Elia amekwisha kuja, nao hawakumtambua, wakamtendea yote, waliyoyataka. Hivyo hata Mwana wa mtu atateswa nao.[#Mat. 14:9-10.]
13Hapo ndipo wanafunzi walipojua, ya kuwa amewaambia mambo ya Yohana Mbatizaji.[#Luk. 1:17.]
14Walipofika penye kundi la watu, mtu akamjia, akampigia magoti, akasema:
15Bwana, umhurumie mwanangu! Kwani ni mwenye kifafa, aumia vibaya. Kwani mara nyingi huanguka motoni, tena mara nyingi huanguka majini.
16Nikampeleka kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.
17Yesu akajibu akisema: Enyi wa kizazi kisichomtegemea Mungu kwa kupotoka! Nitakuwapo nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni hapa, nilipo![#5 Mose 32:5; Yoh. 14:9.]
18Yesu alipomkaripia, pepo akamtoka; naye mtoto akapona tangu saa ileile.
19Kisha wanafunzi wakamjia Yesu, alipokuwa peke yake, wakasema: Mbona sisi hatukuweza kumfukuza huyo?[#Mat. 10:1.]
20Naye akawaambia: Ni kwa ajili hammtegemei Mungu vema. Maana nawaambia la kweli: Cheo chenu cha kumtegemea Mungu kikiwa kidogo kama kipunje cha mbegu, mtauambia mlima huu: Ondoka hapa, ulipo, uende pale! nao utaondoka. Hivyo halitakuwako neno lisilowezekana nanyi.[#Mat. 21:21; Luk. 17:6; 1 Kor. 13:2.]
21Lakini kabila hili la pepo halitoki isipokuwa kwa nguvu ya kuomba na ya kufunga.
22Walipokuwa wakizunguka huko Galilea, Yesu akawaambia: Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwa watu,
23nao watamwua, kisha siku ya tatu atafufuliwa. Wakasikitika sana.
24Walipofika Kapernaumu, watoza kodi wakamjia Petero, wakasema: Mfunzi wenu halipo kodi?[#2 Mose 30:13.]
25Akasema: Hulipa. Naye alipokuja nyumbani, Yesu akaanza kumwuliza akisema: Waonaje, Simoni, wafalme wa nchi huwatoza watu gani chango au kodi? Wana wao wenyewe au wageni?
26Alipojibu: Huwatoza wageni, Yesu akamwambia: Basi, wana wenyewe hawatozwi.
27Lakini tusiwakwaze! Nenda pwani, uloe kwa ndoana! Kisha samaki wa kwanza atakayezuka umshike, ufumbue kinywa chake! Mle utaona fedha, itwae, ukawape kwa ajili yetu, mimi na wewe!