Mateo 20

Mateo 20

Vibarua katika shamba.

1*Ufalme wa mbingu umefanana na mtu mwenye numba aliyetoka mapema kutafuta wakulima, wamlimie mizabibu yake.[#Mat. 21:33.]

2Alipokwisha patana na wakulima mchana kutwa kwa shilingi akawatuma katika mizabibu yake.

3Ilipopata saa tatu, akatoka, akaona wengine waliosimama sokoni pasipo kazi.

4Nao akawaambia: Nendeni nanyi katika mizabibu! Nami kinachowapasa nitawapani.

5Basi, wakaenda. Ilipopata saa sita na saa kenda, akatoka tena, akafanya vilevile.

6Hata ilipopata saa kumi na moja, akatoka, akaona wengine waliosimama, akawaambia: Mnasimamaje hapa mchana kutwa pasipo kazi?

7Wakamwambia: Kwa sababu hakuna mtu aliyetuita kazini. Akawaambia: Nendeni nanyi katika mizabibu!

8Basi ilipokuwa jioni, mwenye mizabibu akamwambia msimamizi wake: Waite wakulima, uwape mshahara wao, uanzie wa mwisho, uishilizie wa kwanza!

9Wakaja wa saa kumi na moja, wakapokea kila mtu shilingi.

10Walipokuja wa kwanza wakadhani, ya kuwa watapokea zaidi. Lakini nao wakapokea kila mtu shilingi.

11Walipoipokea wakamnung'unikia mwenye nyumba[#Luk. 17:10.]

12wakisema: Hawa wa mwisho wamefanya kazi saa moja tu, nawe umewalinganisha na sisi tuliosumbuka kwa kazi na kwa jua kali mchana kutwa.

13Naye akamjibu mmoja wao akisema: Mwenzangu, sikukupunja, hukupatana nami kwa shilingi?

14Chukua iliyo yako, ujiendee! Huyu wa mwisho nataka kumpa kama wewe.

15Kumbe sina ruhusa ya kufanya na mali yangu mwenyewe, kama nitakavyo? Au jicho lako linakuwa baya, kwa sababu mimi ni mwema?[#Rom. 9:16-21.]

16Hivyo ndivyo, walio wa mwisho watakavyokuwa wa kwanza, nao walio wa kwanza watakuwa wa mwisho. Kwani waalikwao ni wengi, lakini wachaguliwao ni wachache tu.*[#Mat. 19:30; 22:14.]

Mwana wa mtu atateswa.

(17-19: Mar. 10:32-34; Luk. 18:31-33.)

17Yesu alipotaka kupanda kwenda Yerusalemu akawachukua wale kumi na wawili, wawe peke yao. Akawaambia njiani:

18Tazameni tunapanda kwenda Yerusalemu. Huko Mwana wa mtu atatiwa mikononi mwao watambikaji wakuu na waandishi, nao watamhukumu, auawe;[#Mat. 16:21; 17:22-23.]

19kwa hiyo watamtia mikononi mwa wamizimu, wapate kumfyoza na kumpiga viboko na kumwamba msalabani. Naye siku ya tatu atafufuliwa.

Yakobo na Yohana.

(20-28: Mar. 10:35-45.)

20Ndipo, alipomjia mama yao wana wa Zebedeo pamoja na wanawe, akamwangukia na kumwomba kitu.[#Mat. 10:2.]

21Alipomwuliza: Wataka nini? akamwambia: Sema, hawa wanangu wawili wakae katika ufalme wako mmoja kuumeni, mmoja kushotoni kwako![#Mat. 19:28.]

22Yesu akajibu akisema: Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kukinywa kinyweo, nitakachokinywa mimi? Walipomwambia: Twaweza,[#Mat. 26:39; Yoh. 18:11; Luk. 12:50.]

23akawaambia: Kinyweo changu mtakinywa, lakini kumketisha mtu kuumeni na kushotoni kwangu hii si kazi yangu, ila hupewa walioandaliwa na Baba yangu.[#Tume. 12:2; Ufu. 1:9.]

24Wenzao kumi walipoyasikia wakawakasirikia hao ndugu wawili.[#Luk. 22:24-26.]

25Lakini Yesu akawaita, wamjongelee, akasema: Mnajua: wafalme wa mataifa huwatawala, nao wakubwa huwatumikisha kwa nguvu.

26Kwenu ninyi visiwe hivyo ila mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu sharti awe mtumishi wenu![#Mat. 23:11; 1 Kor. 9:19.]

27Naye anayetaka kuwa wa kwanza kwenu sharti awe mtumwa wenu![#Mar. 9:35.]

28Kama Mwana wa mtu asivyokuja, atumikiwe, ila amekuja kutumika na kuitoa roho yake kuwa makombozi ya watu wengi.[#Luk. 22:27; Fil. 2:7; 1 Tim. 2:6; Ebr. 9:12-14.]

Vipofu wawili.

(29-34: Mar. 10:46-52; Luk. 18:35-43.)

29Walipokuwa wakotoka Yeriko, likamfuata kundi la watu wengi.

30Ndipo, vipofu wawili waliokaa njani kando waliposikia, ya kuwa ni Yesu anayepita, wakapaza sauti wakisema: Bwana, mwana wa Dawidi, tuhurumie!

31Lakini watu wakawakaripia, wanyamaze. Lakini wao wakazidi kupaza sauti wakisema: Bwana, mwana wa Dawidi, tuhurumie!

32Ndipo, Yesu aliposimama, akawaita, akasema: Mwataka, niwafanyie nini?

33Wakamwambia: Bwana, twataka, macho yetu yafumbuke!

34Yesu akawaonea uchungu, akawagusa macho yao. Mara wakapata kuona, wakamfuata.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania