The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Yesu alipoyamaliza maneno hayo yote, akawaambia wanafunzi wake:[#Mat. 20:18; 2 Mose 12:1-20.]
2Mmejua, baada ya siku mbili itakuwa Pasaka; naye Mwana wa mtu atatolewa, awambwe msalabani.
3Hapo watambikaji wakuu na wazee wa huko kwao wakakusanyika nyumbani mwa mtambikaji mkuu, jina lake Kayafa,
4wakala njama ya kumkamata Yesu kwa werevu wapate kumwua.
5Lakini walisema: Kwanza sikukuu ipite, watu wasije, wakafanya fujo!
6Yesu alipokuwa Betania nyumbani mwa Simoni Mkoma,
7akamjia mwanamke mwenye kichupa cheupe cha jiwe kilichojaa mafuta ya maua yaliyo yenye bei kubwa. Akammiminia kichwani pake, alipokaa akila.
8Lakini wanafunzi walipoviona wakachukiwa, wakasema: Upotevu huu ni wa nini?
9Kwani mafuta haya yangaliwezekana kuuzwa kwa fedha nyingi, wakapewa maskini.
10Lakini Yesu alipovitambua, akawaambia: Mbona mnamsikitisha mwanamke huyu? Maana amenitendea tendo zuri.
11Kwani maskini mnao kwenu siku zote, lakini mimi hamwi nami siku zote.[#5 Mose 15:11.]
12Kwani alipoyamimina mafuta haya, aupake mwili wangu, ameutengenezea kuzikwa.
13Kweli nawaambiani: Po pote katika ulimwengu wote, patakapotangazwa Utume huu mwema, patasemwa nacho hiki, alichokitenda yeye, naye akumbukwe.
14Hapo wale kumi na wawili mwenzao mmoja aliyeitwa Yuda Iskariota akaenda kwa watambikaji wakuu,
15akasema: Mwataka kunipa nini, nitakapomtia mikononi mwenu? Wakaagana kumpa fedha 30.[#Zak. 11:12; Yoh. 11:57.]
16Toka hapohapo alitafuta njia iliyofaa amtoe.[#1 Tim. 6:9-10.]
17Siku ya kwanza ya kula mikate isiyotiwa chachu wanafunzi wakamjia Yesu wakisema: Unataka, tukuandalie wapi, uile kondoo ya Pasaka?[#Mat. 26:2; 2 Mose 12:18-20.]
18Naye akasema: Nendeni mjini kwa fulani, mmwambie: Mfunzi anasema: Siku zangu zinatimia! Kwako nitaila kondoo ya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.[#Mat. 21:3.]
19Wanafunzi wakafanya, kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa kondoo ya Pasaka.
(20-30: Mar. 14:17-26; Luk. 22:14-23; Yoh. 13:21-30.)20Ilipokuwa jioni, akakaa chakulani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
21Walipokuwa wakila, akasema: Kweli nawaambiani: Mwenzenu mmoja atanichongea.
22Wakasikitika sana, wakaanza kumwuliza kila mmoja: Bwana, ni mimi?
23Naye akajibu akisema: Aliyetowelea pamoja nami bakulini ndiye atakayenichongea.
24Mwana wa mtu anakwenda njia yake, kama alivyoandikiwa; lakini yule mtu, ambaye Mwana wa mtu atachongewa naye, atapatwa na mambo. Ingalimfalia yule mtu, kama asingalizaliwa.
25Ndipo, Yuda aliyemchongea alipomwuliza akisema: Mfunzi mkuu, ni mimi? Akamjibu: Ndio umesema.
26Walipokuwa wakila, Yesu akatwaa mkate, akauombea, akaumega, akawapa wanafunzi akisema: Twaeni, mle! Huu ndio mwili wangu.[#Mat. 14:19; 1 Kor. 11:23-26.]
27Kisha akatwaa kinyweo, akashukuru, akawapa akisema: Nyweni nyote humu!
28Maana hii ndiyo damu yangu ya Agano Jipya inayomwagwa kwa ajili ya wengi, wapate kuondolewa makosa.[#2 Mose 24:8; Yer. 31:31-34; Zak. 9:11.]
29Lakini nawaambiani: Tangu sasa sitayanywa tena mazao ya mizabibu mpaka siku ile, nitakapoyanywa mapya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.
(30-35: Mar. 14:27-31; Luk. 22:31-34.)30Walipokwisha kuimba wakatoka kwenda mlimani pa michekele.[#Sh. 115—118; Luk. 22:39; Yoh. 18:1.]
31Hapo Yesu akawaambia: Usiku huu wa leo ninyi nyote mtajikwaa kwangu kwani imeandikwa:
32Nitampiga mchungaji, kondoo wa kundi lake watawanyike; lakini nitakapokwisha kufufuliwa nitawatangulia kwenda Galilea.[#Mat. 28:7.]
33Ndipo, Petero alipojibu akimwambia: Ijapo wote wajikwae kwako, lakini mimi sitajikwaa kamwe.
34Yesu akamwambia: Kweli nakuambia: Usiku huu wa leo jogoo atakapokuwa hajawika, utakuwa umenikana mara tatu.[#Yoh. 13:38.]
35Petero akamwambia: Hata ijaponipasa kufa pamoja nawe, sitakukana kabisa. Nao wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.[#Mat. 26:56.]
36Kisha Yesu akaenda pamoja nao mahali panapoitwa Getisemane. Akawaambia wanafunzi: Kaeni hapa, niende kule, niombe!
37Akamchukua Petero na wale wana wawili na Zebedeo, akaanza kusikitika na kuhangaika,[#Ebr. 5:7.]
38akawaambia: Roho yangu inaumizwa sana na masikitiko, imesalia kufa tu. Kaeni papa hapa, mkeshe pamoja nami![#Sh. 43:5; Yoh. 12:27.]
39Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akaomba akisema: Baba, ikiwezekana kinyweo hiki kinipite, nisikinyuwe! Lakini yasifanyike, kama nitakavyo mimi, ila yafanyike kama utakavyo wewe![#Yoh. 10:17-18; 18:11; Ebr. 5:8.]
40Alipowajia wanafunzi, akawakuta, wamelala usingizi, akamwambia Petero: Hamkuweza kukesha pamoja nami saa moja tu?
41Kesheni na kuomba, msije kuingia majaribuni! Roho inataka kuitikia, lakini mwili ni mnyonge.[#Ebr. 2:14; 4:15.]
42Akaenda tena mara ya pili, akaomba akisema: Baba, isipowezekana, hiki kinipite, nisikinywe, basi, uyatakayo wewe na yafanyike![#Mat. 6:10.]
43Alipokuja tena, akawakuta, wamelala usingizi, kwani macho yao yalikuwa mazito.
44Akawaacha, akaenda tena, akaomba mara ya tatu akisema tena maneno yale yale.[#2 Kor. 12:8.]
45Kisha akawajia wanafunzi, akawaambia: Mwafuliza kulala usingizi, uchovu uwatoke? Tazameni, saa iko karibu, Mwana wa mtu atiwe mikononi mwa wakosaji![#2 Sam. 24:14.]
46Inukeni, twende! Tazameni, mwenye kunichongea yuko karibu![#Yoh. 14:31.]
47Angali akisema, mara akaja Yuda, mmoja wao wale kumi na wawili, pamoja na watu wengi sana wenye panga na rungu waliotoka kwa watambikaji wakuu na kwa wazee wa huko kwao.
48Lakini mwenye kumchongea alikuwa amewapa kielekezo akisema: Nitakayemnonea ndiye, mkamateni!
49Mara akamjia Yesu, akasema: Salamu, mfunzi mkuu! Akamnonea.
50Yesu akamwambia: Mwenangu, umejia nini? Ndipo, walipokuja, wakamkamata Yesu kwa mikono yao, wakamfunga.
51Papo hapo wale waliokuwako pamoja na Yesu mmoja wao akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumwa wa mtambikaji mkuu, akamkata sikio.
52Ndipo, Yesu alipomwambia: Urudishe upanga wako mahali pake! kwani wote wenye kushika panga wataangamizwa kwa upanga.[#1 Mose 9:6; Ufu. 13:10.]
53Au unadhani: Siwezi kumbembeleza Baba yangu, naye akaniletea sasa hivi malaika wengi kupita elfu kumi na mbili?
54Lakini Maandiko yangetimizwaje yale ya kwamba, sharti yawe vivyo hivyo?
55Saa ile Yesu akawaambia yale makundi ya watu: Mmetoka wenye panga na rungu, mnikamate mimi, kama watu wanavyomwendea mnyang'anyi. Kila siku nilikaa hapa Patakatifu nikifundisha, lakini hamkunikamata.
56Lakini haya yote yamekuwapo, Maandiko ya Wafumbuaji yatimizwe. Papo hapo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.[#Mat. 26:31.]
(57-75: Mar. 14:53-72; Luk. 22:54-71; Yoh. 18:12-27.)57Lakini wale waliomkamata Yesu wakampeleka kwa mtambikaji mkuu Kayafa; ndiko, walikokusanyika waandishi na wazee.
58Lakini Petero akamfuata mbalimbali, mpaka akafika uani kwa mtambikaji mkuu, akaingia ndani akakaa pamoja na watumishi, uone mwisho.
59Lakini watambikaji wakuu na baraza ya wakuu wote wakamtafutia Yesu ushuhuda wa uwongo, wapate kumwua.
60Lakini hawakuupata, ingawa walikuja mashahidi wa uwongo wengi, lakini hawakumshinda.
61Halafu wakaja wawili, wakasema: Huyu amesema: Nina nguvu ya kulivunja Jumba la Mungu na kulijenga tena muda wa siku tatu.[#Yoh. 2:19-21.]
62Ndipo, mtambikaji mkuu alipoinuka, akamwambia: Hujibu neno, hawa wanayokusimangia?
63Lakini Yesu akanyamaza kinya. Mtambiakaji mkuu akamwambia: Ninakuapisha na kumtaja Mungu Mwenye uzima, utuambie, kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu![#Mat. 27:12.]
64Yesu akamwambia: Wewe ulivyosema, ndivyo. Tena nawaambiani: Tangu sasa mtamwona Mwana wa mtu, anavyokaa kuumeni kwa nguvu, tena atakavyokuja juu ya mawingu ya mbinguni.[#Mat. 16:27; 24:30; Luk. 21:27; Sh. 110:1; 68:35; Dan. 7:13.]
65Ndipo, mtambikaji mkuu alipozirarua nguo zake, akasema: Amekwisha kumbeza Mungu. Mashahidi tunawatakia nini tena? Tazameni, sasa hivi mmesikia, anavyombeza Mungu.[#Mat. 9:3; Yoh. 10:30,33.]
66Mwaonaje? Nao wakajibu, wakasema: Amepaswa na kufa.[#3 Mose 24:16; Yoh. 19:7.]
67Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi[#Yes. 50:6.]
68wakisema: Tufumbulie, Kristo: ni nani aliyekupiga?
69Naye Petero alikuwa nje, amekaa uani. Kijakazi mmoja akamjia, akasema: Hata wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilea.
70Akakana mbele yao wote akisema: Sijui unayoyasema.
71Alipotoka uani na kufika mlangoni, mwingine akamwona, akawaambia wale waliokuwako: Huyu alikuwa pamoja na Yesu na Nasareti.
72Akakana tena na kuapa akisema: Simjui mtu huyo.
73Punde kidogo wakamjia Petero waliosimama pale, wakamwambia: Kweli, na wewe u mwenzao, kwa maana matamko yako yanakutambulisha.
74Ndipo, alipoanza kujiapiza na kuapa akisema: Simjui mtu huyo! Mara hiyo jogoo akawika.
75Hapo Petero akalikumbuka lile neno la Yesu, aliposema: Jogoo atakapokuwa hajawika, utakuwa umenikana mara tatu. Akatoka nje, akalia sana kwa uchungu.[#Mat. 26:34.]