The chat will start when you send the first message.
1Mimi Paulo niliyefungwa kwa ajili yake Kristo Yesu na ndugu yetu Timoteo tunakusalimu wewe, Filemoni, uliye mpendwa wetu na mwenzetu wa kazi.[#Ef. 3:1.]
2Tunakusalimu na wewe, Apia, uliye dada yetu, na wewe, Arkipo, uliye mwenzetu wa kupiga vita. Tunawasalimu nao wateule wote waliomo nyumbani mwako.[#Kol. 4:17.]
3Upole uwakalie na utengemano unaotoka kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo![#Rom. 1:7.]
4Namtolea Mungu wangu shukrani siku zote nikikukumbuka katika kuomba kwangu.
5Kwani nimesikia, unavyompenda Bwana Yesu na kumtegemea, hata unavyowapenda watakatifu wote.
6Nakuombea, hivyo, tulivyo mmoja kwa kumtegemea Mungu, vikupe nguvu ya kutambua kwamba: Mema yote, mlio nayo, sharti mmrudishie Kristo![#Fil. 1:9.]
7Kwani twalifurahi sana, mioyo yetu ikatulia kwa ajili ya upendo wako, maana roho za watakatifu umezipatia kituo wewe, ndugu yangu.[#2 Kor. 7:4.]
8Kwa hiyo, ijapo Kristo anipe moyo mkuu wa kukuagiza likupasalo,
9kwa ajili ya ule upendo wako nataka kukubembeleza tu. Tazama mimi Paulo nilivyo! Ni mzee, tena hata sasa mfungwa wake Kristo Yesu.
10Nakubembeleza kwa ajili ya mtoto wangu, niliyemzaa humu kifungoni mwangu; ndiye Onesimo[#1 Kor. 4:15; Gal. 4:19; Kol. 4:9.]
11asiyekufalia kale, lakini sasa anatufalia sana, wewe hata mimi.
12Nikimrudisha kwako, ni kama nitautuma moyo wangu mwenyewe, ukufikie.
13Nami nalitaka kumshika, akae kwangu, akufanyizie kazi hii ya kunitumikia humu kifungoni, nilimotiwa kwa ajili ya kuutangaza Utume mwema.[#Fil. 2:30.]
14Lakini kwa kuwa hujaweza kuitikia, sikutaka kufanya kitu, kusudi wema wako usiwe wa kushurutishwa, ila uwe wa kupendezwa mwenyewe.[#2 Kor. 9:7.]
15Kwani labda kwa sababu hii ametengwa nawe siku chache, upate kuwa naye kale na kale.
16Tena sasa siye kama mtumwa tu, ila apita mtumwa kwa kuwa hata ndugu mpendwa; kweli mimi nampenda, nawe utanipita kwa kumpenda, maana ni wako kwanza kimtu, tena ni wako Kikristo.[#1 Tim. 6:2.]
17Basi, kama waniwazia kuwa mwenzio, mpokee yeye kama mimi!
18Lakini kama kiko chako, alichokipotoa, au kama yuko na deni kwako, hayo nibandikie mimi!
19Mimi Paulo nimeviandika hivi kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitayalipa. Sitakuambia: U mdeni wangu mimi, deni lako ni moyo wako.
20Kweli, ndugu yangu, nataka kuona upato kwako, maana u wake Bwana. Upatie moyo wangu kituo kwake Kristo![#File. 7.]
21Nimekuandikia, kwa sababu nimejipa moyo wa kwamba: Utatii, tena najua, ya kuwa utafanya kuyapita yale, niliyoyasema.
22Kisha nitengenezee chumba cha kufikia! Kwani kingojeo hiki ninacho cha kwamba: Mtanipata tena kwa ajili ya kuomba kwenu.[#Fil. 1:25; 2:24.]
23Wanakusalimu akina Epafura aliyefungwa pamoja nami kwa ajili ya Kristo Yesu[#Kol. 1:7; 4:12.]
24na Marko na Aristarko na Dema na Luka walio wenzangu wa kazi.[#Kol. 4:10,14.]
25Upole wa Bwana Yesu Kristo uzikalie roho zenu! Amin.