The chat will start when you send the first message.
1Sifa njema ina kima kuliko mali nyingi,
upendeleo nao hufaa kuliko fedha na dhahabu.
2Mkwasi na maskini hukutana,
aliyewaumba wote wawili ni Bwana.
3Mwerevu akiona mabaya hujificha,
lakini wajinga hupita tu, wakapatwa nayo.
4Mapato ya unyenyekevu na ya kumcha Bwana
ni mali na macheo na uzima.
5Miiba na matanzi yamo katika njia ya mpotovu,
ajiangaliaye hujiepusha hapo.
6Mfundishe mtoto, apate kuijua njia yake,
asiiache, hata atakapokuwa mzee.
7Mkwasi huwatawala maskini,
naye akopaye ni mtumishi wake amkopeshaye.
8Apandaye uovu huvuna mapotovu,
nayo fimbo iliyomtia ukali itakomeshwa.
9Atazamaye wengine kwa jicho lenye utu hubarikiwa,
kwani humgawia mnyonge chakula chake.
10Mfukuze mfyozaji! Ndipo, ugomvi nao utakapotoka,
ndipo, mteto nayo matusi yatakapokoma.
11Apendaye, moyo utakate, naye mwenye midomo ipendezayo
huwa rafiki yake mfalme.
12Macho ya Bwana humlinda mwenye ujuzi,
lakini maneno yake avunjaye agano huyapindua.
13Mvivu husema: Simba yuko nje,
nitauawa peupe barabarani.
14Vinywa vya wanawake wa wengine ni mashimo marefu,
Bwana anayemchukia, utumbukia humo.
15Ujinga umefungiwa moyoni mwa mtoto,
lakini fimbo ya kumchapa itautoa mwake.
16Amkorofishaye mnyonge humpatia mali nyingi,
amgawiaye mwenye mali humpunguzia mali zake.
17Litege sikio lako, uyasikilize maneno ya werevu wa kweli!
Nao moyo wako uuelekezee ujuzi wangu!
18Kwani ni mazuri ya kuyaangalia mwako ndani,
yote pamoja yawe tayari kutumiwa na midomo yako.
19Kwa kwamba: Bwana na awe kimbilio lako,
kwa hiyo ninakufundisha leo wewe mwenyewe.
20Je? Sikukuandikia mambo makuu,
yakupe mashauri mema ya kukujulisha maana?
21Ndiyo yatakayokujulisha maongozi ya kweli na maneno ya kweli,
upate kuwajibu maneno ya kweli wao waliokutuma.
22Usimnyang'anye mnyonge! Kwani ni mnyonge,
wala mwenye mateso usimkanyage mlangoni!
23Kwani Bwana huwagombea, wakigombezwa na watu,
nao wanaowapokonya huwapokonya roho zao.
24Usifanye bia na mtu mwenye moyo mdogo,
wala usitembee na mtu mwenye makali kama ya moto,
25kusudi usijizoeze mwenendo wake,
ukajipatia tanzi la roho yako.
26Usiwe nao wanaopeana mikono
wakijitoa kuwa dhamana za wengine kwa ajili ya madeni yao!
27Usipoweza kulipa halafu,
mbona wakichukue kitanda chako, unachokilalia?
28Usisogeze mawe ya mipaka ya kale,
baba zako walioyayaweka!
29Ukiona mtu ajihimizaye kazi zake, atakwenda kutumikia wafalme,
asitumikie watu walio watuwatu tu.