Mashangilio 110

Mashangilio 110

Utume wa Mungu kwa mfalme wake.

(Taz. Mat. 22:44; Tume. 2:34-35; Ebr. 1:13; 5:6.)

1*Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti kuumeni kwangu, mpaka niwaweke adui zako chini miguuni pako![#1 Kor. 15:25; Fil. 2:8-9; Ebr. 10:12-13.]

2Bakora yako ya kifalme yenye nguvu Bwana ataituma toka Sioni: Katikati ya adui zako tawala wewe![#Sh. 2:6.]

3Walio ukoo wako watakutokea kwa kupenda wenyewe siku iyo hiyo, utakapokwenda vitani; hapo watakuwa wamevaa mapambo yapasayo Patakatifu. Wana wako watazaliwa, kama umande unavyozaliwa asubuhi mapema.[#Sh. 29:2.]

4Bwana aliapa, naye hatajuta: Wewe u mtambikaji wa kale na kale, kama Melkisedeki alivyokuwa.*[#1 Mose 14:18-20; Ebr. 5:10; 6:20; 7:17,21.]

5Bwana alioko kuumeni kwako atawaponda wafalme; itakuwa siku hiyo, makali yake yatakapotokea.[#Sh. 2:2,5,9.]

6Atakapohukumu kwenye wamizimu, ndipo, mizoga yao itakapojaa, akiwaponda vichwa mahali palipo papana.[#Dan. 2:32-38.]

7Atakunywa maji ya mtoni huko njiani, kwa hiyo atakiinua kichwa chake.[#Fil. 2:8-9.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania